RUWASA yaagizwa kutatua kero ya maji hospitali ya Ngara

KAGERA: Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, ambaye ni Mlezi wa Mkoa wa Kager, ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya tathmini ya haraka na kubaini mahitaji halisi ya kuunganisha huduma ya maji katika Hospitali ya Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

Agizo hilo amelitoa kufuatia ombi la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Samira Khalfani, aliyeomba Serikali kuingilia kati changamoto ya ukosefu wa maji katika hospitali hiyo ili kupunguza adha wanayopata wagonjwa, hususan wanawake wanaokwenda kujifungua.

Samira amewasilisha ombi hilo leo Agosti 9, mbele ya Waziri Kijaji wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji Mdogo wa Rulenge, Wilaya ya Ngara.

Amesema Serikali tayari imetatua kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ngara kwa kuhakikisha wilaya hiyo inapata Hospitali ya Wilaya, hivyo changamoto iliyobaki ni kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa na huduma ya maji ya uhakika.

“Wanawake wengi wananunua maji mtaani pindi wanapolazwa, wanakuja na maji yao. Tunaomba Serikali ije na mpango maalumu wa kuondoa changamoto hiyo haraka ili kupunguza maangaiko kwa wagonjwa na watumiaji wa hospitali hiyo,” amesema Samira.

Kwa upande wake, Waziri Kijaji amesisitiza umuhimu wa RUWASA kufanya tathmini hiyo kwa haraka ili kubaini mahitaji ya miundombinu na kuchukua hatua za kuhakikisha Hospitali ya Wilaya ya Ngara inaunganishwa na huduma ya maji.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo, pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinatolewa katika mazingira yenye huduma muhimu za msingi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button