Costech yaipa SUA jukumu wafugaji Kongwa

DODOMA; TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imetoa ufadhili wa Sh milioni 400 kwa ajili ya Mradi wa kuimarisha uwezo wa wafugaji kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa na Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ikilenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa malisho kwa wafugaji nyakati za kiangazi.
Mradi huo unatekelezwa katika Wilaya ya Kongwa ,mkoani Dodoma , wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu .
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu, amesema hayo baada ya kutembelea shamba darasa la malisho na kuanglia matokeo ya uwekezaji ambao Serikali imefanya kupitia mfugaji wa Kata ya Mtanana , wilaya ya Kongwa , mkoani Dodoma.

Dk Nungu amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 36 inayotekelezwa nchini, ambapo serikali ilitoa Sh bilioni 19 na mradi huo mmoja umepatiwa sh milioni 400 kwa ufadhili wa COSTECH, ili kupata suluhisho za athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kuwa dira ya 2050 imeweka matamanio makubwa yakiwemo ya Taifa liwe linasafirisha mifugo ubora na nyama na kuuzwa nje ya nchi .
Amesema kupitia mradi huo kinachoangaliwa na COSTECH ni kuona mkulima na mfugaji aweze kupata malisho mwaka mzima na kusiwe na changamoto yoyote.
“ Leo tupo shambani kwenye shamba darasa kuangalia matokeo , tumeona kutoka kwenye sera na sasa yamekuja shambani kwa mkulima na mfugaji , sera imesema na dira imesema mkulima awe ananufaika matokeo ya utafiti “ amesema Dk Nungu.

Dk Nungu amesema matokeo ya utafiti hivi sasa yanawafikia wananchi wa kawaida , na mradi huo kilelekezo kupitia kwa mfugaji mmoja ambapo nyuma yake wanaonufaika ni wafugaji na wakulima zaidi ya 1,300 wa kata ya Mtanana ,wilayani Kongwa.
“ Tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizi bilioni 19 si jambo la mchezo bali imedhamiria kuona Dira ya 2050 iweze kufikiwa,” amesema Dk Nungu.
Naye Mkuu wa Mradi huo, Profesa Sebastian Chenyambuga kutoka SUA, amesema mradi huo umelenga kuimarisha uwezo wa wafugaji kuwa na malisho yenye kustahimili ukame na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzalisha malisho na kuondoa migogoro baina yao na wakulima.

Profesa Chenyambuga amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitatu na ulianza Oktoba mwaka jana (2025) .
Kwa upande wake Mfugaji wa Kijiji cha Mtanana ,Clement Alphonce amesema wataalamu wa SUA walikuwakutanisha wakulima na wafugaji na kupatiwa mafunzo ya namna ya kulima malisho ya mifugo.
“ Baada ya mafunzo nikavutiwa na teknolojia hii, nimelima ekari mbili za malisho na nilikuwa na ng’ombe 56 wa kienyeji ,nimeuza 54 na kubakiza wawili , fedha yake kinanunua ng’ombe wakisasa 14 wenye kutoa maziwa mengi kuanzia lita tano hadi 22 kwa siku , tofauti na niliokua nao awali wakitoa nusu lita kwa siku, “ amesema Alphonce.



