Costech yaipa SUA jukumu wafugaji Kongwa

DODOMA; TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imetoa ufadhili wa Sh milioni 400 kwa ajili ya Mradi wa kuimarisha uwezo wa wafugaji  kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi  unaotekelezwa na Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),  ikilenga  kutatua changamoto ya upatikanaji wa malisho kwa wafugaji nyakati za kiangazi.

Mradi huo unatekelezwa katika Wilaya ya Kongwa ,mkoani Dodoma , wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu .

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu, amesema hayo baada ya kutembelea shamba darasa la malisho na kuanglia matokeo ya uwekezaji ambao Serikali imefanya kupitia mfugaji wa  Kata ya Mtanana , wilaya ya Kongwa , mkoani Dodoma.

Dk Nungu amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 36  inayotekelezwa nchini, ambapo serikali ilitoa Sh bilioni 19  na mradi huo mmoja umepatiwa sh milioni 400 kwa ufadhili wa COSTECH,  ili kupata suluhisho za athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa  dira ya 2050  imeweka matamanio  makubwa  yakiwemo ya  Taifa liwe linasafirisha mifugo ubora na nyama  na kuuzwa nje ya nchi .

Amesema kupitia mradi huo kinachoangaliwa na COSTECH  ni kuona mkulima na mfugaji aweze  kupata malisho mwaka mzima na kusiwe na changamoto  yoyote.

“ Leo tupo shambani kwenye shamba darasa  kuangalia matokeo , tumeona kutoka kwenye sera  na sasa yamekuja shambani  kwa mkulima na mfugaji  , sera imesema na dira imesema  mkulima awe ananufaika  matokeo ya utafiti “ amesema Dk Nungu.

Dk Nungu amesema matokeo ya utafiti hivi sasa yanawafikia  wananchi wa kawaida , na  mradi huo kilelekezo  kupitia kwa mfugaji mmoja ambapo  nyuma yake wanaonufaika  ni wafugaji na wakulima zaidi ya 1,300 wa kata ya Mtanana ,wilayani Kongwa.

“  Tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizi  bilioni 19 si jambo la mchezo bali imedhamiria kuona  Dira ya 2050 iweze kufikiwa,” amesema Dk Nungu.

Naye Mkuu wa Mradi huo, Profesa Sebastian Chenyambuga kutoka SUA, amesema mradi huo umelenga kuimarisha uwezo wa wafugaji kuwa na malisho yenye kustahimili ukame na  athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzalisha malisho na kuondoa  migogoro baina yao   na wakulima.

Profesa Chenyambuga  amesema kuwa  mradi huo utatekelezwa kwa  miaka mitatu na  ulianza  Oktoba mwaka jana (2025) .

Kwa upande wake Mfugaji wa Kijiji cha Mtanana ,Clement Alphonce amesema wataalamu wa SUA  walikuwakutanisha wakulima na wafugaji na  kupatiwa mafunzo   ya namna ya kulima malisho ya mifugo.

“  Baada ya mafunzo nikavutiwa na teknolojia hii, nimelima ekari mbili za malisho na  nilikuwa na ng’ombe 56 wa kienyeji ,nimeuza  54 na kubakiza wawili , fedha yake kinanunua ng’ombe wakisasa 14  wenye kutoa maziwa mengi  kuanzia  lita tano hadi  22  kwa siku , tofauti na niliokua nao awali wakitoa nusu lita kwa siku,  “ amesema Alphonce.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button