Bodaboda Chunya sasa waja kivingine

MBEYA; Waendesha bodaboda wilaya ya chunya ,mkoani mbeya wameanza kuchukua hatua za kujenga mfumo wa pamoja wa kiuchumi,kwa kuanzisha Mfuko Maalumu wa Bodadoda kwa ajili ya kusaidiana na kuanzisha miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Bodaboda Wilaya ya Chunya, Chance Mwaitambo amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa kifedha kundi hilo na kupunguza utegemezi wanapokumba na changamoto,huku wakipanga kuanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa(SACCOS)itakayowezesha kukopeshana kwa masharti nafuu.
Mwaitambo amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mfuko Maalumu wa Bodaboda wilaya ya Chunya,akieleza kuwa kila mwanachama atachangia Sh 20000 kwa mwezi.

Amesema fedha hizo zitatumiaka kusaidia wanachama wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali,ikiwemo ajali,matibabu na hata kifo, lakini mfuko huo haulengi kutatua changamoto za wanachama pekee bali ni sehemu ya uwekezaji.
“Mpango huu pia ni hatua ya kuweka msingi wa uwekezaji wa pamoja,kwani baadae tunatarajia kuanzisha miradi ya uzalishaji itakayoongeza mapato na kuufanya mfuko kuwa endelevu na kuwa chombo cha maendeleo ya kiuchumi kwetu,”amesema Mwaitambo.
Akizindua mfuko huo Mkuu wa Wilaya ya Chunya ,Mbaraka Batenga amewataka wanachama kuwa na katiba na kuhakikisha wanaifahamu ili kila mmoja ajue haki na wajibu wake.

Amewataka pia wanachama kuzingatia masharti ya mfuko,akisisitiza kuwa mwanachama ambaye hatatekleza wajibu wa kuchangia hatanufaika na mfuko huo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Kelvin Nshishi amewataka waendesha bodaboda hao kuhakikisha mfuko huo hauwi chanzo cha migogoro huku akionya mwendokasi kuwa ni miongoni wa sababu zilizochangia ajali na kupoteza maisha ya vijana wengi.



