Wafungwa Ukonga kupimwa magonjwa yasiyoambukiza

DAR ES SALAAM; WAFUNGWA 600 wa Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, wanatarajiwa kupatiwa huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo moyo, katika kambi maalumu ya afya iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Tukio hilo ni sehemu ya mkakati wa JKCI kufikia wananchi walipo na kuongeza fursa za uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yakigundulika mapema huwezesha mgonjwa kupata matibabu kwa wakati.
Katika kambi hiyo, wafungwa wanapimwa afya ya moyo pamoja na vipimo vingine, ikiwamo ECG, ECHO na vipimo vya damu, huku wale watakaobainika kuwa na changamoto za kiafya wakipatiwa matibabu au rufaa kwa uchunguzi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema kambi hiyo ilianza Agosti 10 na kuhitimishwa Agosti 13,2026.
Amebainisha kuwa wafungwa watakaohitaji matibabu watapatiwa dawa, wakati wale watakaohitaji uchunguzi wa kibingwa zaidi watapelekwa JKCI kwa huduma zaidi.

“Wale ambao watahitaji rufaa watakwenda katika taasisi yetu waweze kuhudumiwa zaidi. Na wale ambao watapata matibabu tutawapatia dawa pale pale walipo,” amesema.
Amesema uchunguzi huo hautaishia Gereza la Ukonga, bali JKCI ina mpango wa kuwafikia wafungwa katika magereza mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza na Mkuu wa kitengo cha Afya wa Jeshi la Magereza, Nsajigwa Mwankenja, amesema huduma hiyo ni muhimu kwa kuwa wafungwa na mahabusu ni sehemu ya raia wa Tanzania na wana haki ya kupata huduma za afya.
Amesema Jeshi la Magereza linashukuru JKCI kwa kuwajumuisha wafungwa katika huduma za uchunguzi wa afya, akisisitiza umuhimu wa kinga na ugunduzi wa mapema wa magonjwa.
“Ni muhimu wafungwa kupata huduma za afya kwa sababu siku moja wanamaliza vifungo vyao na kurejea uraiani, mfungwa anayerejea katika jamii akiwa na afya njema ataweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa taifa, tofauti na anayerejea akiwa na matatizo makubwa ya kiafya.



