Serikali yajizatiti kukabili magonjwa yasiyoambukiza

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kuimarisha huduma za kinga, uhamasishaji na elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, Dk. Omary Ubuguyu, katika Mkutano wa 13 wa Afya Leo unaofanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, taasisi za umma na binafsi, wataalamu pamoja na wananchi.

Dk. Ubuguyu amesema udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza hauishii katika kutoa elimu pekee, bali unahitaji mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwemo kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya pombe na kuzingatia ulaji unaofaa kwa kuongeza matumizi ya matunda na mboga.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa licha ya hali ya mazoezi kuimarika katika baadhi ya maeneo, bado kuna changamoto ya watu kutofanya shughuli za kutosha za mwili kutokana na matumizi ya vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji, huku matumizi ya pombe miongoni mwa vijana yakiongezeka.

Aidha, amesema hatua nyingine muhimu ni kuimarisha utambuzi wa mapema wa magonjwa hayo, akieleza kuwa ongezeko la umri wa kuishi kwa Watanzania kutoka wastani wa miaka 48 hadi zaidi ya miaka 68 limeongeza umuhimu wa kuwabaini mapema watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Dk. Ubuguyu amesema bado kuna changamoto ambapo watu wengi hugundulika wakiwa tayari katika hatua za kati au za juu za ugonjwa, jambo linaloongeza gharama za matibabu na kuathiri nguvu kazi ya taifa.

Amesisitiza wananchi kuanza kupima afya zao kabla ya kuonesha dalili, sambamba na kubadili mtindo wa maisha na kuzingatia huduma za kinga, akisema hatua hizo ni muhimu katika kupunguza mzigo wa magonjwa hayo kwa mtu mmoja mmoja, familia na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Kaushik Ramaiya, amesema wameandaa kitabu kinachoitwa Mtindo wa Maisha, kitakachosaidia jamii kuelewa namna bora ya kuishi na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Amesema kitabu hicho pia kitasaidia watu ambao tayari wanaishi na magonjwa hayo kuelewa hatua wanazoweza kuchukua ili kuboresha maisha yao.

Nao washiriki wa mkutano huo wanaoishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Pascalina Ngwanda na Samwel Maingu, wamesema changamoto kubwa zinazowakabili ni gharama za dawa hospitalini pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu magonjwa hayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button