Komakundi uhunzi kwao ni urithi, ajira, utamaduni

KILIMANJARO; KIJIJI cha Komakundi, Kata ya Mamba Kaskazini, shughuli ya uhunzi si kazi ya kawaida tu, bali ni urithi wa vizazi, chanzo cha ajira na sehemu muhimu ya utamaduni wa jamii.

Kwa mujibu wa maelezo ya wenyeji, maarifa ya kufua na kutengeneza chuma yamekuwepo katika eneo hili kwa zaidi ya miaka 300.

Hadithi ya wenyeji inaeleza kwamba, miaka mingi iliyopita, mwanamke aliyekuja kutoka Afrika Magharibi akiwa mkimbizi alifika katika eneo hili na kuwafundisha wenyeji maarifa ya kutengeneza chuma.

Tangu wakati huo, ujuzi huo umekuwa ukipitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine hadi leo.

Leonard Ngowi, Diwani wa Kata ya Mamba Kaskazini mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, anasema alikuta shughuli hiyo ikiendelea tangu utotoni.

“Toka tumezaliwa, tulikuta hii kazi. Babu zetu ndio waliowafundisha baba zetu. Mimi nilikuwa namfuatilia babu yangu wakati anaendelea na hiyo kazi. Hata mimi najua kazi hii na ninaweza kuifanya,” anasema.

Kwa sasa, shughuli hiyo inaendelezwa kupitia Komakundi Blacksmiths, kikundi kinachoongozwa na mwenyekiti wake, Ombaristo Makundi, ambaye pia ni kiongozi wa kikundi hicho kilichopo Mamba Kaskazini.

Kwa Ombaristo Makundi na wanachama wenzake, Komakundi Blacksmiths si karakana pekee, bali ni mahali ambapo historia, maarifa ya jadi na teknolojia ya mikono vinaendelea kuishi na kupewa nafasi katika uchumi wa jamii.

            Kutoka udongo wenye chuma hadi chuma cha kufua

Anasema uzalishaji wa chuma katika historia ya eneo hili ulihusisha kutumia udongo wenye chembechembe za chuma uliopatikana maeneo ya Pare. malighafi hiyo ilichakatwa kwa kutumia moto mkali na mkaa ili kupata chuma ambacho baadaye kilifuliwa na kutengenezwa kuwa zana mbalimbali.

“Leo, teknolojia imebadilika kwa kiasi, lakini msingi wa kazi bado ni uleule: moto, hewa, joto, chuma na ustadi wa fundi.

“Katika tanuru, mkaa huwashwa na hewa huingizwa kwa nguvu kupitia mfumo wa compressor. Hewa hiyo huongeza nguvu ya moto na kufanya joto lifikie kiwango kinachoweza kulainisha na kuchakata chuma.

“Fundi hutambua chuma kimepata joto linalofaa kwa kuangalia hali yake ambapo chuma huingizwa kwenye moto na kutolewa mara kadhaa.

“Baada ya kupata joto linalohitajika, huwekwa juu ya sehemu ya kufulia na kugongwa kwa nyundo hadi kupata umbo linalotakiwa na hapo ndipo sayansi ya uhunzi inapokutana na uzoefu wa fundi,” anasema Makundi.

Kila chuma kina kazi yake

Komakundi Blacksmiths hutengeneza bidhaa mbalimbali kulingana na mahitaji ya wateja na ukubwa wa oda. Miongoni mwa bidhaa hizo ni majembe, rato, mapanga na mikuki.

Pia hutengeneza vifaa vya ujenzi, bidhaa za mapambo na bidhaa zinazoweza kutumika katika sekta ya utalii. Vifaa hivyo hutengenezwa kwa oda maalum, huku malighafi zikichaguliwa kwa umakini kulingana na aina ya bidhaa inayotakiwa.

Kwa mfano, spring za magari chakavu zinaweza kutumika kutengeneza mapanga na rato, rods za chuma hutumika kutengeneza mikuki, huku mabamba ya chuma yenye unene unaofaa yakitumika kutengeneza majembe.

Hivyo, karakana hii pia ni mfano wa uchumi wa mzunguko, ambapo chuma kutoka kwenye magari na vifaa vilivyotumika kinaweza kurejeshwa na kupewa matumizi mapya.

Ujuzi hnaogawanywa kwa Hatua

Ujenzi wa zana hauishii kwenye tanuru. Kuna mgawanyo wa kazi unaofanya uzalishaji uweze kuendelea kwa ufanisi kwani wapo wanaohusika na kuandaa na kuendesha moto, wengine huingiza na kutoa chuma kwenye tanuru, wengine hushikilia chuma, kukigonga na kukipa umbo, huku wengine wakinoa na kukamilisha bidhaa. Pia kuna wanaotengeneza na kuweka mipini.

Baada ya bidhaa kukamilika, baadhi hupelekwa sokoni na nyingine husambazwa kwa wateja wanaokuja moja kwa moja kwenye karakana.

Kwa sasa, kikundi kina zaidi ya watu 20 wanaohusika moja kwa moja katika shughuli hizi, huku wanawake wakichangia pia katika usambazaji na biashara ya bidhaa.

Zana zinazowasaidia wakulima

Moja ya sababu kubwa zinazofanya uhunzi huu kuwa muhimu kwa jamii ni uhusiano wake wa moja kwa moja na kilimo. Wakulima hutumia zana zinazotengenezwa hapa katika kulima, kupalilia na kuhudumia mazao kama mahindi na maharage.

Kwa wakazi wa maeneo ya jirani, upatikanaji wa zana hizi karibu nao hupunguza gharama na usumbufu wa kutafuta zana mbali.

Leonard Ngowi anaeleza kwamba zana zinazotengenezwa na mafundi wa Komakundi zinaaminiwa na wenyeji kwa sababu ya uimara wake.

Anatoa mfano wa rato zinazotengenezwa kwa kutumia spring za magari yaliyokwisha kutumika. Kwa uzoefu wake, zana hizo zinaweza kuwa imara zaidi kuliko baadhi ya zana za bei nafuu zinazopatikana sokoni.

Kwa hiyo, uhunzi wa Komakundi hauzalishi bidhaa pekee, bali pia unasaidia uzalishaji wa chakula na shughuli za kila siku za wakulima.

           Wamasai na soko la utamaduni

Soko la bidhaa za Komakundi halipo kwa wakulima pekee. Wamasai kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Arusha na Ngorongoro, ni miongoni mwa wateja muhimu.

Mikuki na bidhaa nyingine za asili bado zina nafasi katika maisha na utamaduni wa jamii ya Wamasai. Hii imeifanya Komakundi kuwa sehemu ambayo ujuzi wa jadi unaendelea kupata soko kupitia utamaduni.

Bidhaa zinazotengenezwa hapa pia huingia kwenye hoteli na maeneo ya utalii kama mapambo na vitu vinavyowakilisha utamaduni wa Afrika Mashariki.

Hivyo, kila bidhaa inayotoka kwenye moto wa tanuru inaweza kuwa na safari ndefu: kutoka kwa fundi, kwenda kwa mkulima, mwanajamii au mfanyabiashara, hadi hoteli au hata kwa mtalii anayesafiri nayo kwenda nyumbani.

   Soko na daraja la fursa,utalii

Watalii wa ndani na wa kimataifa wanapofika katika eneo hili, hawaji tu kununua bidhaa, bali pia huangalia mchakato mzima wa uhunzi, huuliza maswali, hujifunza historia na kuona kwa macho namna chuma kinavyobadilishwa kutoka kipande cha malighafi kuwa bidhaa yenye matumizi.

Wageni hao pia huleta mawazo mapya kuhusu bidhaa zinazoweza kutengenezwa kwa ajili ya masoko ya utalii.

Kwa jamii, hii ni fursa ya kugeuza urithi wa jadi kuwa chanzo cha kipato na wakati huohuo kuutangaza utamaduni wa eneo hilo.

Sehemu ya mapato yanayotokana na shughuli hizi inaweza pia kuchangia maendeleo ya kijiji na kuboresha maisha ya wananchi.

 Ajira na maisha ya familia

Kwa watu wanaofanya kazi hapa, uhunzi ni kazi inayowawezesha kuendesha maisha yao. Mapato yanayotokana na kazi hii yamesaidia familia kugharamia mahitaji mbalimbali, ikiwemo elimu ya watoto, ujenzi wa nyumba, ufugaji na mahitaji ya kila siku.

Kwa mtazamo wa jamii, mafanikio makubwa si mtu mmoja kuwa na kipato, bali kuona familia zinaweza kupeleka watoto shule kutokana na kazi hii.

Kwa vijana, shughuli hii inaweza kuwa chanzo cha ajira na pia njia ya kujifunza ujuzi wa vitendo unaoweza kuendelezwa kwa maisha yote.

Miongoni mwa vijana wanaofanya kazi ya uhunzi ni Elvis Makundi, ambaye anasema alijifunza kazi hiyo kutoka kwa baba yake aliyekuwa akifanya shughuli hiyo kwa miaka mingi.

Kupitia baba yake, Elvis alipata nafasi ya kujifunza ujuzi na uzoefu unaohitajika katika kazi ya uhunzi.

Elvis anasema uhunzi ni kazi kama kazi nyingine na hakuna sababu ya vijana kuiona kuwa ni kazi isiyofaa. Anawashauri vijana wenzake kuingia katika kazi hiyo na kuitumia kama fursa ya kujipatia kipato na kujenga maisha yao.

Kwa mujibu wa Elvis, uhunzi hauna tofauti na kazi nyingine, hivyo vijana wanapaswa kuondokana na dhana kwamba baadhi ya kazi hazina thamani na kuhimiza vijana wenzake kuthamini kazi za mikono na kujifunza ujuzi ambao unaweza kuwasaidia kujitegemea.

   Changamoto ya mazingira

Pamoja na mafanikio hayo, uhunzi wa Komakundi unakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya mkaa. Tanuru linahitaji joto kubwa, hivyo mafundi hutumia mkaa wa kuni. Hali hii inaweza kuchangia ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.

Leonard Ngowi anaona kwamba serikali na wadau wanapaswa kusaidia kutafuta teknolojia mbadala ambayo inaweza kupunguza utegemezi wa mkaa wa miti.

Moja ya njia anazotaja ni matumizi ya mkaa wa mawe, lakini anasisitiza kwamba hilo linahitaji vifaa na teknolojia maalum.

Hivyo, si suala la kubadilisha aina ya mkaa pekee, bali linahitaji uwekezaji katika teknolojia salama, yenye ufanisi na inayolinda mazingira.

 Changamoto ya Urithi wa Kizazi

Changamoto nyingine ni namna ya kuhakikisha ujuzi huu unaendelea kuwepo.

Baadhi ya vijana hawaonyeshi hamu kubwa ya kuingia katika kazi ya uhunzi, jambo linaloweza kuhatarisha urithi huu endapo wazee wenye ujuzi hawatapata warithi wa kuwafundisha.

Hata hivyo, fursa ya utalii, soko la zana za kilimo na mahitaji ya bidhaa za jadi vinaweza kuifanya kazi hii ivutie zaidi kwa kizazi kipya.

Kinachohitajika ni kuunganisha ujuzi wa jadi na teknolojia ya kisasa ili vijana waone kuwa uhunzi si kazi ya zamani pekee, bali ni fursa ya biashara .

Akiwa mwenyekiti wa Komakundi na kiongozi wa Komakundi Blacksmiths, Ombaristo Makundi ni sehemu ya uongozi unaosimamia mwendelezo wa shughuli za uhunzi katika eneo la Mamba Kaskazini.

Chini ya uongozi wa kikundi, uhunzi unaendelea kuwa sehemu ya maisha ya jamii, huku ukitoa nafasi kwa watu kujifunza ujuzi, kuzalisha bidhaa na kujipatia kipato.

Uongozi wa kikundi una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha maarifa haya hayaishii kwa kizazi cha sasa pekee, bali yanaendelea kufundishwa na kutumiwa na vijana.

Kuwepo kwa viongozi kama Ombaristo Makundi, pamoja na mafundi wenye uzoefu na vijana wanaojifunza kazi hiyo, kunaweza kusaidia kujenga daraja kati ya urithi wa jadi na mahitaji ya soko la kisasa.

Komakundi Blacksmiths ni urithi unaoweza kuwa kesho

Hadithi ya Komakundi Blacksmiths ni hadithi ya moto unaowaka zaidi ya tanuru.

Ni hadithi ya mababu waliorithisha ujuzi kwa watoto wao, ya mafundi wanaogeuza chuma chakavu kuwa zana mpya, ya wakulima wanaotumia majembe na rato zao mashambani, ya Wamasai wanaonunua mikuki na bidhaa za asili na ya watalii wanaofika kujifunza na kununua bidhaa za mikono, pia ni hadithi ya jamii inayojitafutia maisha kupitia ujuzi wake wenyewe.

Kwa sasa, kinachohitajika si kuacha teknolojia hii, bali kuiboresha kwa kupata nishati inayolinda mazingira, kuboresha vifaa vya kazi, kuwafundisha vijana, kutafuta masoko mapya na kuunganisha uhunzi na utalii wa kiutamaduni.

Komakundi Blacksmiths inaweza kuwa mfano wa namna urithi wa jadi unavyoweza kugeuzwa kuwa ajira, biashara, utalii na maendeleo ya jamii bila kupoteza utambulisho wake.

Moto wa tanuru unaweza kuzimwa jioni, lakini ujuzi unaotengenezwa ndani yake unaweza kuendelea kuwaka kwa vizazi vijavyo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button