Mambo yameiva Dodoma mkutano wazee wanaume

DAR ES SALAAM; CHAMA cha Wazee Wanaume Tanzania kinatarajia kufanya mkutano wake wa kwanza jijini Dodoma Agosti 29, mwaka huu, ukilenga kujadili changamoto zinazowakabili ikiwamo matunzo, afya na ustawi wao.

Mkutano huo utakaoshirikisha wajumbe 200 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Akizungumza jijini Dodoma, Mwenyekiti wa chama hicho, Peter Mavunde, alisema mkutano huo utakuwa ni fursa kwa wazee wanaume kujadili masuala yanayowahusu na kuweka mikakati ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Alisema chama hicho kinalenga kuwaunganisha wazee wanaume, kushiriki katika malezi ya vijana kimaadili, kutunza tunu za taifa na kuchangia shughuli za maendeleo na ustawi wa jamii.

Mavunde alisema mkutano huo pia utajadili upatikanaji wa huduma za afya na matibabu, pamoja na changamoto za baadhi ya wazee kukosa matunzo kutokana na watoto wao kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kulinda na kuimarisha ustawi wa wazee nchini, akisema msisitizo huo unapaswa kuungwa mkono kwa utekelezaji wa sera na sheria zinazolinda maslahi yao.

Mavunde alisema mkutano huo utaimarisha pia mshikamano wa wazee wanaume na kuainisha namna bora ya kutumia uzoefu na taaluma zao katika maendeleo ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button