Wabuni vigae vya ukutani kwa kutumia chupa za plastiki

TANGA; Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimeendelea kujipambanua kama kitovu cha tafiti na bunifu zinazotoa majibu ya moja kwa moja kwa changamoto zinazoikabili jamii, huku kikisisitiza mfumo wa vitendo kwa wanafunzi wake kabla ya kuhitimu.
Akizungumzia juhudi hizo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, amesema chuo kimeimarisha mfumo ambapo kila muhula wanafunzi wanafanya miradi ya vitendo chini ya usimamizi wa wahadhiri na kuiteetea kama sehemu ya mitihani yao.
“Kila muhula wanafunzi wanasimamiwa na kufanya miradi chini ya usimamizi wa walimu, na wanazitetea kama sehemu ya mitihani yao,” anaeleza Profesa Liwa, akisisitiza kuwa mbinu hiyo inawafanya wahitimu kuwa na uelewa mpana katika kutatua changamoto za kiutendaji.
Katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira inayotokana na taka ngumu, Chuo Kikuu cha Ardhi kimeleta tija kupitia uvumbuzi mpya wa kutengeneza vigae vya ukutani (wall tiles) vinavyotokana na chupa za plastiki.

Mwanamapinduzi wa wazo hili ni Isabellah Edwin Sam, mwanafunzi wa mwaka wa nne chuoni hapo, ambaye alibaini kuwa chupa za plastiki za rangi zimekuwa zikitupwa kwa wingi kutokana na bei yake kuwa chini, hali inayochochea uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Ili kupunguza kadhia hiyo, Isabellah alibuni mbinu ya kuchakata taka hizo na kuzigeuza kuwa vigae imara vinavyoweza kutumika katika ujenzi wa kuta, hususan katika maeneo ya bafu na vyoo.
Akizungumzia ubora wa uvumbuzi wake, Isabellah ameeleza kuwa bidhaa hiyo ni thabiti na inaendelea kuboreshwa zaidi.
Amesema hatua inayofuata ni kuwasilisha vigae hivyo katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kupata uthibitisho rasmi kabla ya kuanza kutumika kwa wingi katika soko la ujenzi.



