SBL yaongeza kasi upatikanaji maji nchini

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendelea kuongeza kasi katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii nchini Tanzania kupitia mpango wake wa “Water for Life”, unaolenga kusaidia jamii zinazokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Kupitia mpango huo, SBL imewekeza zaidi ya shilingi bilioni mbili katika utekelezaji wa miradi 32 ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kuwanufaisha zaidi ya watu milioni 2.3 kwa kuwawezesha kupata maji safi na salama pamoja na kuboresha afya na mazingira yao.

SBL imesema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha shughuli za kampuni zinaenda sambamba na kuleta matokeo chanya kwa jamii, hususan katika maeneo ya vijijini ambako changamoto ya miundombinu ya maji imekuwa ikiathiri afya, usafi na shughuli za kiuchumi.

Mpango wa “Water for Life” pia unalenga kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu ya maji unaendelea kuwa na manufaa kwa muda mrefu kwa kuhusisha jamii katika kutunza, kusimamia na kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kufanya kazi.

Hatua hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wanawake na watoto, ambao katika maeneo yenye uhaba wa maji mara nyingi hutumia muda mwingi kutafuta maji. Upatikanaji wa maji karibu na makazi yao unawawezesha kutumia muda huo kwa shughuli za kiuchumi, elimu na majukumu mengine ya maendeleo.

Mbali na kujenga miundombinu ya maji, SBL imekuwa ikiwahusisha wanawake katika juhudi za kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha usafi wa mazingira. Zaidi ya wanawake 100 wamewezeshwa kupitia mpango wa “Water Champions”, wakipewa elimu, maarifa na ujuzi wa kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa maji, usafi na matumizi salama ya maji.

Kwa mujibu wa taarifa za SBL, kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maji, ikiwemo Serikali na taasisi zinazohusika na huduma za maji. Miradi ya aina hiyo imekuwa ikilenga maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma ya maji.

SBL imeeleza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama hauishii katika kujenga vituo vya maji pekee, bali unahitaji jamii kuwa na uelewa wa namna ya kutunza miundombinu, kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kupatikana kwa vizazi vijavyo.

Hatua hiyo inaendana na msisitizo wa umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi, Serikali na jamii katika kutatua changamoto za huduma muhimu za kijamii. Kwa SBL, mpango wa “Water for Life” ni sehemu ya safari yake ya kuwekeza katika jamii na kuchangia maendeleo endelevu nchini.

Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa SBL imefikia hatua ya kukamilisha mradi wake wa 30 wa maji nchini, huku mradi wa Baray, Karatu, ukiwanufaisha zaidi ya wakazi 15,000.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button