Wito watolewa kudhibiti mifugo inayoharibu mashamba

MTWARA: VIONGOZI mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ikiwemo watendaji kata wametakiwa kudhibiti uvamizi wa mifugo inayoingia kwenye maeneo ya wakulima kwani inaleta kero kwa wakulima hao.

Hayo yamejiri leo Agosti 28, 2026 wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Mtwara kuhusu kujadili taarifa za hesabu za mwisho za halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Richard Mwalingo, amesema kwenye maeneo yao hawajatenga maeneo kwa ajili ya mifugo hivyo inazalisha kero baina ya wakulima na wafugaji kwani wanafahamu wana wakulima wanaofanya shughuli zao za kilimo cha mboga mboga na bustani lakini pia mazao ya msimu.

‘’Watendaji kata kuhakikisha kwamba mifugo inapoingia kuchukua hatua za haraka siyo mpaka kusubiri mifugo imefika inakaa miaka miwili mitatu inaanza kuleta kero zinazoweza kusema twende ofisi ya mkuu wa wilaya, ukileta kwenye ofisi yetu nitakuuliza wewe umefanya nini…’’amesisitiza Mwalingo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikoa hicho ambaye pia ni diwani wa kata ya Dihimba Hassan Salamata amesema maagizo hayo yote yaliyotolewa na kaimu mkuu huyo wa wilaya ikiwemo suala hilo la udhibiti wa mifugo wataenda kuyafanyika kazi ili kuleta ufanisi wa uzalishaji wa mazao hayo na mengine.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Vijijini Nashir Mfaume mbali na hilo amewapongeza na kuendelea kuwaomba madiwani pamoja na watalaamu wa halmashauri kuendelelea kufanya kazi vizuri ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.

“Kwasababu ni matakwa ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona fedha zinazoletwa kwenye halmashauri zinaenda kumaliza changamoto za wananchi lakini pia tuendelee kuwa na mahusiano mazuri kwasababu bila mshikamano mzuri hatuwezi kufanya kazi vizuri’’amesema Nashir

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button