Mwenge wa Uhuru wazindua kituo janja cha maji Bukoba

KAGERA: Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zimezindua Kituo Janja cha Maji katika Kata ya Ijuganyondo, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, ambacho kinatumika kwa mfumo wa kidijitali na kusaidia kupunguza upotevu wa maji.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Michael Wazo Mwang’onda, amewaomba wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.

Amesema Mradi wa Kituo Janja cha Maji unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kata ya Ijuganyondo, ambapo unalenga kuhudumia zaidi ya wananchi 700 kwa kuwawezesha kupata huduma ya maji safi na salama.
Mwang’onda amesema mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, kwa kuwa upatikanaji wa maji safi na salama unachangia moja kwa moja katika kuimarisha afya ya jamii, usafi wa mazingira, kupunguza muda unaotumika kutafuta maji pamoja na kuongeza fursa za wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Ijuganyondo wameeleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo, wakibainisha kuwa upatikanaji wa huduma ya maji karibu na makazi yao utawasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji na kuboresha mazingira ya maisha ya jamii.
Taarifa iliyosomwa na Mhandisi kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), Edmund Deus, imeeleza kuwa ujenzi wa Kituo Janja umetokana na upanuzi wa mtandao wa mradi wa maji unaohudumia Kata za Ijuganyondo na Karabagaine.

Amesema uzinduzi wa Kituo Janja cha Maji ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na muhimu za kijamii, sambamba na kuimarisha miundombinu inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuchochea maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenge wa Uhuru 2026 unaendelea kuangaza njia ya maendeleo, huku kupitia miradi kama Kituo Janja cha Maji, wananchi wakishuhudia matokeo ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za msingi na kuinua maisha ya Watanzania, kwa kuzingatia kaulimbiu ya Mwenge Kitaifa mwaka huu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane.”



