Jengo ESAMI kuongeza ufanisi mafunzo ya viongozi Afrika

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema ujenzi wa jengo jipya la ghorofa tatu lenye thamani ya dola za Marekani 750,000 katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Usimamizi cha Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), ni utekelezaji wa maamuzi ya Bodi ya Taasisi hiyo yenye lengo la kuongeza ufanisi katika kuwaandaa viongozi wa umma na sekta binafsi.
Mkomi amesema hayo leo baada ya kuzindua ujenzi wa jengo hilo katika hafla iliyofanyika eneo la ujenzi la ESAMI, akieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, hivyo uwepo wa jengo hilo utaongeza uwezo wa kutoa huduma kwa nchi za Afrika.
Amesema majengo yaliyopo kwa sasa hayakidhi mahitaji kutokana na ongezeko la mahitaji ya mafunzo, huku akieleza kuwa ESAMI ilijengwa miaka 50 iliyopita.

Mkomi, ambaye ni mjumbe pekee wa Tanzania katika Bodi ya ESAMI na kuiwakilisha nchi katika uzinduzi huo, amesema jengo hilo litakuwa na madarasa, ofisi za utawala pamoja na miundombinu mingine muhimu, hatua ambayo itaongeza thamani ya taasisi hiyo yenye wanachama 10 barani Afrika.
Amesema ujenzi huo ni miongoni mwa makubaliano ya Bodi, kwa kuwa ESAMI ni taasisi inayotoa mafunzo ya uongozi kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, hivyo ni wajibu kuhakikisha jengo hilo linajengwa kwa hadhi ya kitaifa na kimataifa.
Mkomi ameitaka Menejimenti ya ESAMI kusimamia kwa karibu ujenzi huo ili utekelezwe kwa kuzingatia maazimio ya Bodi, viwango vya kimataifa na kukamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa hakutakiwi kuwepo visingizio vya ucheleweshaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Profesa Peter Kiuluku, amesema ujenzi wa jengo hilo ni uwekezaji muhimu wenye lengo la kuongeza idadi ya viongozi wenye maadili na dhamira ya kupambana na rushwa kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.

Kiuluku amesema dhamira hiyo inaendana na maono ya mwanzilishi wa taasisi hiyo, Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi wenye maadili katika kuleta maendeleo.
Amesema Afrika inahitaji kuwekeza zaidi katika elimu pamoja na miundombinu ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya kisasa katika ujenzi wa majengo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Naye Msimamizi na Mshauri wa Mradi huo, Abdulrazak Kapwani, kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Kapwani, amesema ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja na utazingatia viwango vya kisasa vilivyowekwa kwenye mkataba.
Kapwani amesema hakuna visingizio vitakavyotumika kuchelewesha ujenzi huo na kwamba mradi utakamilika ndani ya muda uliopangwa.




My relatives always say that I am killing my time here at net, however I know I am getting experience every day by reading thes nice content.