Wananchi 5,000+ wanufaika mradi wa maji Bumai

KAGERA: Zaidi ya wananchi 5,000 wa Kijiji cha Bumai, chenye vitongoji 14 katika Kata ya Kishanje, wilayani Bukoba, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji baada ya kukamilika kwa Mradi wa Maji Bumai wenye thamani ya Sh milioni 870.5.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amezindua mradi huo huku akiwaomba wananchi kutunza miundombinu ya maji na kulinda miradi inayotekelezwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Amesema Serikali inalenga kuboresha huduma ya maji katika vijiji vyote nchini kwa kufikia asilimia 85, pamoja na kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa huduma hiyo moja kwa moja majumbani, hatua itakayowasaidia kutumia muda mwingi katika shughuli za maendeleo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Evaristo Mugaya, mradi huo umekamilika na wananchi sasa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amesema shughuli zilizotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tanki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji, vituo 11 vya kuchotea maji, uunganishaji wa maji katika kaya 100, ujenzi wa mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita, mnara wa mita tisa, matenki ya kukusanyia maji pamoja na ujenzi wa ofisi za CBWSO.
Ameeleza kuwa mradi huo umetokana na ukusanyaji wa maji kutoka kwenye chemchemi zilizopo katika vitongoji vya Buhinda na Bugandika.
Mugaya amesema kukamilika kwa mradi huo kumepunguza changamoto ya magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara katika Kijiji cha Bumai na vijiji jirani, kutokana na upatikanaji wa maji safi na salama.



