Rika la Erumeruasi lapewa pongezi ujenzi kituo cha afya

RIKA la Erumeruasi katika jamii ya Watemi, Kata ya Oldonyosambu, Tarafa ya Sale wilayani Ngorongoro, limepongezwa kwa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Oldonyosambu chenye thamani ya Sh milioni 305.411, hatua inayoonesha namna mila na tamaduni zinavyoweza kutumika kuchochea maendeleo na kuboresha huduma za jamii.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Hamza Husein Hamza, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, amesema juhudi hizo ni mfano wa kuigwa na jamii nyingine, akisisitiza kuwa mila na tamaduni zinapounganishwa na maendeleo zinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za jamii zinazolenga kuboresha huduma za msingi, hususan afya, huku akieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ilichangia Sh milioni 80 katika ujenzi wa kituo hicho.

Hamza amelipongeza Rika la Erumeruasi kwa kutumia misingi ya mshikamano na uwajibikaji wa kijamii katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo ya jamii.

Katika harambee iliyoambatana na sherehe hizo, wananchi na wadau walichangisha Sh milioni 184.493 kwa ajili ya mahitaji ya kituo hicho, ikiwemo vifaa tiba na vitendanishi.

Kituo hicho kinatarajiwa kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususan wanawake wajawazito ambao kwa muda mrefu walilazimika kwenda Digodigo au Engaresero kwa ajili ya kujifungua.

Hatua hiyo inaonesha kuwa mila ya kushirikiana na kuchangia maendeleo inaweza kuzaa matokeo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, hasa katika huduma muhimu kama afya.

Sherehe hizo pia ziliambatana na makabidhiano ya uongozi na majukumu ya kijamii kutoka Rika la Erumeruasi kwenda Rika la Erumashili, huku Pius Maroseck akikabidhiwa jukumu la kuongoza rika hilo.

Makabidhiano hayo yanaakisi umuhimu wa mila za jamii ya Watemi (Wasonjo) katika kurithisha majukumu, heshima, amani na mshikamano kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, huku vijana wakihimizwa kutumia misingi hiyo kuendeleza maendeleo ya jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button