Watu 2,750 wapatiwa matibabu ya macho Z’bar

ZAIDI ya watu 2,700 wamepatiwa matibabu ya macho katika Kambi Maalum ya Matibabu ya Macho inayoendeshwa Zanzibar na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku wagonjwa 256 wakifanyiwa upasuaji wa macho.
Kambi hiyo inayofanyika kwa ushirikiano kati ya MNH, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Qatar Charity, imeendelea kutoa huduma mbalimbali katika Kituo cha Afya Sebuleni, Mkoa wa Mjini Magharibi. Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya macho, dawa, miwani kwa wananchi wenye uhitaji pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo.
Takwimu hizo zinaonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kambi hiyo, ambayo ilianza Agosti 29 na inatarajiwa kuhitimishwa Septemba 4, 2026. Hadi sasa wananchi zaidi ya 985 walikuwa tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kupata huduma, huku timu ya wataalamu ikiendelea kuwahudumia wananchi waliojitokeza.
Akizindua huduma hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Hassan Khamis Hafidh, amepongeza ushirikiano kati ya MNH, Qatar Charity na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema umewezesha wananchi kusogezewa huduma za kibingwa karibu na maeneo yao.
“Ushirikiano kati ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Qatar Charity na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeleta huduma za kibingwa karibu na wananchi wetu. Hii ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya,” amesema Hafidh.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Macho kutoka MNH, Dk Joachim Kilemile, amesema hospitali imejipanga kuhakikisha wananchi wote wanaofika kambini wanapata huduma licha ya idadi kubwa ya waliojitokeza.
“Tunawaomba wananchi wasikate tamaa kutokana na idadi kubwa ya waliojitokeza. Muhimbili imejipanga kwa wataalamu na vifaa vya kutosha kuhakikisha kila mgonjwa anayefika kambini anapata huduma stahiki, ikiwemo upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo,” amesema Dk Kilemile.
Amesema upasuaji wa mtoto wa jicho unafanyika kwa kutumia gari maalum la upasuaji, jambo linalowezesha huduma hizo za kibingwa kutolewa karibu na wananchi. SOMA: Wagonjwa 823 kufanyiwa upasuaji macho



