Katambi awasamehe wasanii,atoa onyo kali

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali imewafutia makosa baadhi ya wasanii na watengeneza maudhui mtandaoni waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu na maadili.

Akizungumza leo, Katambi amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya wasanii na watengeneza maudhui hao kupewa nafasi nyingine ya kujirekebisha, huku wakishiriki semina ya maadili ili kuwawezesha kuelewa wajibu wao kwa jamii na Taifa.

Amesema Serikali inalenga kuwapa nafasi ya kutumia vipaji na majukwaa yao kwa njia yenye manufaa kwa jamii, badala ya kutengeneza maudhui kwa lengo la kupata watazamaji wengi na malipo bila kuzingatia madhara yanayoweza kujitokeza. “Usiweke kontenti ili tupate view ili ulipwe bila kujali kuwa unaleta athari kwenye jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Katambi.

Aidha, Katambi ametoa onyo kali kwa wasanii na watengeneza maudhui, akisema baada ya wito huo, yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. “Baada ya wito huu, yeyote atakayevunja sheria atachukuliwa hatua za kisheria kama hawezi kujenga maadili ya Taifa letu,” amesema. SOMA: Yvonne Chakachaka kutoa elimu ya hakimiliki kwa wasanii

Waziri Katambi pia amewataka wananchi na wadau wa sanaa kutoa taarifa katika mamlaka husika pale wanapoona msanii au mtengeneza maudhui amekiuka sheria, badala ya kuchukua hatua wenyewe. “Msanii anapokosea, mpeleke sehemu husika na atahudumiwa kulingana na sheria husika,” amesema.

Hata hivyo, Katambi amesema Jennifer Jovin ‘Niffer’ Noel na Anko T bado hawajafutiwa makosa yao kwa kuwa hawajafika kuonana naye. Amesema wawili hao hawajafika kutokana na kuwa nje ya nchi, ambapo mmoja yuko Rwanda na mwingine China. Hatua hiyo inaendelea kuonesha msisitizo wa Serikali kwa wasanii na watengeneza maudhui kutumia majukwaa yao kwa kuzingatia sheria, maadili na maslahi ya jamii.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button