Serikali yataja mikakati michezo kwa wenye ulemavu

DODOMA; Serikali imetaja hatua mbalimbali inazochukua kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhamasisha michezo kwa watu wenye ulemavu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Septemba 2, 2026 na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Nyamizi Mhoja, aliyehoji serikali ina mkakati gani wa kuendeleza michezo kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuzalisha wachezaji wenye ulemavu
“Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa imeendelea kuhamasisha na kuendeleza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michezo kwa kuandaa makocha wa michezo ya watu wenye ulemavu, kuendesha matamasha ya michezo yanayowajumuisha watu wenye ulemavu.
“Kuendesha mashindano ya ndani ya michezo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu, pamoja na kuwezesha ushiriki wa wanamichezo wenye ulemavu katika mashindano ya kimataifa.
“Vilevile Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa imeendelea kuhamasisha uanzishaji na usajili wa vyama vya michezo kwa watu wenye ulemavu, ili kusaidia katika kusimamia maendeleo ya michezo kwa watu wenye ulemavu, ambapo hadi Agosti 2026, jumla ya vyama tisa vya michezo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu vimesajiliwa ikiwemo mchezo wa soka, mpira wa kikapu, tenisi, riadha na kuogelea,” amesema Waziri Makonda.



