Tamasha la FuTopia kuanza Agosti 2027 Zanzibar

ZANZIBAR: TAMASHA la FuTopia linatarajiwa kurejea Zanzibar kwa toleo lake la tatu, likilenga kuendelea kujenga jukwaa linalowaunganisha watu kupitia muziki, sanaa, utamaduni, ubunifu na mawazo mapya.

Tamasha hilo la siku tatu litafanyika Fumba Town, Zanzibar, kuanzia Agosti 6 hadi 8, 2027, huku waandaaji wakifungua milango kwa wasanii na wabunifu kutoka nyanja mbalimbali kuomba kushiriki.

Mbali na burudani, FuTopia limejikita katika kuibua nafasi za mwingiliano wa kijamii, ambapo hadhira haishii kuwa watazamaji pekee bali inahusishwa katika uzoefu wa kisanii na ubunifu.

Katika toleo la pili, tamasha hilo liliwavuta zaidi ya watu 3,700 ndani ya siku mbili na kuwakutanisha wasanii, wabunifu na washiriki kutoka Tanzania na Zanzibar pamoja na nchi mbalimbali za Afrika na maeneo mengine duniani.

Wasanii waliowahi kushiriki ni pamoja na Bensoul kutoka Kenya, Rosa Ree wa Tanzania, Vania Ice kutoka Burundi, DJ LAG wa Afrika Kusini, Hammer Q kutoka Zanzibar na La Negra Mexa Y Las Cumbiancheras kutoka Mexico.

Kwa waandaaji, utofauti huo wa washiriki unaonyesha namna sanaa inavyoweza kuwa daraja la kuunganisha jamii zenye tamaduni, mitazamo na uzoefu tofauti.

FuTopia pia inatoa nafasi kwa wanamuziki, wacheza ngoma, washairi, wasimuliaji, waigizaji, wasanii wa fani mbalimbali na wabunifu wa maudhui shirikishi kuonyesha vipaji vyao na kujaribu njia mpya za kuwafikia na kuwashirikisha watu.

Mkurugenzi Mkuu wa Busara Promotions, Lorenz Herrmann, alisema jamii imekuwa sehemu muhimu ya safari ya FuTopia na mchango wake umewezesha tamasha hilo kukua.

“Tunawashukuru wote ambao wamekuwa sehemu ya safari ya FuTopia hadi sasa. Wasanii, hadhira, washirika, watu waliojitolea na jamii wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuijenga tamasha hili,” alisema.

Herrmann alisema toleo la tatu litaendelea kutoa nafasi kwa sauti mpya, mawazo mapya na uzoefu wenye maana kwa washiriki.

Kwa mtazamo mpana, kurejea kwa FuTopia Zanzibar kunatoa nafasi kwa wasanii na jamii kukutana, kubadilishana uzoefu na kuonyesha namna sanaa na utamaduni vinavyoweza kuchochea mshikamano, ubunifu na mawasiliano miongoni mwa watu.

Wasanii na wabunifu wanaotaka kuwa sehemu ya toleo hilo wanaweza kutuma maombi kupitia fomu ya ushiriki ya tamasha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button