Bidhaa za Tanzania kufika masoko ya dunia

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imewataka Watanzania na wawekezaji kushirikiana kupitia vyama na vyombo vya wafanyabiashara kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuzitangaza katika masoko ya kimataifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Ephraim Mafuru, wakati wa Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Barani Afrika na Maonesho ya Tatu ya Kilimo, Mifugo na Ufugaji wa Kuku Barani Afrika, yanayofanyika Dar es Salaam.
Amesema maonesho hayo yanalenga kuwaunganisha wafanyabiashara na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi, kubadilishana uzoefu na kutafuta fursa za masoko. “Tanzania tayari inauza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 10 kwa mwaka, lakini ina uwezo wa kufikia Dola bilioni 20 endapo wazalishaji, wafanyabiashara na taasisi zinazohusika wataimarisha ushirikiano” alisema.
Mafuru amesema matarajio ya maonesho hayo, yanayoshirikisha zaidi ya watu 1,000 kutoka nchi 35, yanatarajiwa pia kuzaa mikataba ya biashara na uwekezaji itakayoongeza uzalishaji, masoko na mapato ya taifa. SOMA: Kilimo, mifugo na uvuvi watakiwa kuongeza tija kufikia Dola bilioni 100



