Mapendekezo marekebisho sheria tasnia sukari haya hapa

DODOMA; Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kilimo wa mwaka 2026 (The Agricultural Laws (Amendments) Act, 2026), ambao unapendekeza marekebisho katika Sheria Nne.
Akiwasilisha muswada huo leo Agosti 27, 2027, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amezitaja sheria hizo kuwa ni, Sheria ya Usalama wa Chakula, Sura ya 249, Sheria ya Tasnia ya Mkonge, Sura ya 30, Sheria ya Tasnia ya Sukari, Sura ya 251 na Sheria ya Tasnia ya Chai, Sura ya 275.
“Sehemu ya Nne ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Tasnia ya Sukari, Sura ya 251. Sheria hii ilitungwa mwaka 2001 kwa madhumuni ya kuanzisha Bodi ya Sukari Tanzania na Chuo cha Taifa cha Sukari, kuweka masharti ya kuboresha, kuendeleza na kudhibiti sekta ya sukari pamoja na mambo yanayohusiana na hayo.
“Kifungu cha 15 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuweka sharti la usajili wa viwanda au mitambo ya sukari kwa kuzingatia matumizi au madhumuni ya bidhaa ya sukari inayozalishwa,” amesema.
Waziri Chongolo amesema lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuongeza wigo wa bidhaa za sukari zinazodhibitiwa ili kuboresha ubora wa bidhaa hizo.
“Kifungu cha 18 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kujumuisha sukari iliyosafishwa na sukari ghafi zinazoweza kuingizwa nchini na mtu ambaye tayari ana kiwanda cha kuchakata sukari ghafi kinachofanya kazi kwa lengo la kuzalisha sukari ya matumizi ya viwandani.
“Lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuongeza udhibiti na kukuza uwekezaji katika tasnia ya sukari. Kifungu cha 21 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kutenganisha mkataba wa utekelezaji na leseni ya uingizaji wa sukari nchini.
“Lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuendeleza sharti la mkataba wa utekelezaji kama nyenzo muhimu katika udhibiti wa wazalishaji wa sukari na masharti ya uagizaji wa sukari ghafi (raw sugar) kwa ajili ya uzalishaji wa sukari ya matumizi ya viwandani.
“ Kifungu cha 42 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza wigo wa watu wanaokusudia kufungasha upya sukari inayozalishwa ndani ya nchi katika kiwango kisichozidi ujazo wa gramu 100.
“Marekebisho haya yataruhusu watu ambao si wazalishaji wa sukari waliosajiliwa na Bodi kufanya ufungashaji. Lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuimarisha udhibiti wa shughuli za ufungashaji upya wa sukari ili kulinda ubora na viwango vya sukari,” amesema Waziri Chongolo.



