EADB, TADB zafanya kweli sekta ya kilimo

DAR ES SALAAM; Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), imezindua dirisha maalumu la uwezeshaji wa fedha lenye thamani ya Shilingi bilioni 50, linalolenga kufungua fursa za upatikanaji wa mitaji nafuu kwa wakulima wadogo na wafanyabiashara wadogo katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini Tanzania.
Dirisha hilo hilo limewezeshwa kupitia mkopo wa Shilingi bilioni 50 kutoka EADB kwenda TADB, kwa lengo la kuchechemua uwekezaji, kuongeza tija na thamani katika shughuli za uzalishaji, uchakataji, usindikaji, biashara za mazao ya kilimo na kuweka miundombinu wezeshi ya kufikia masoko kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo ikiwemo mifugo na uvuvi.
Walengwa watawezeshwa mikopo yenye riba nafuu, masharti rafiki na upatikanaji rahisi, itakayowawezesha kuwekeza katika uzalishaji, pembejeo na zana za kisasa, usindikaji, uongezaji thamani, uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko, kwa mujibu wa vigezo vya bidhaa.
Dirisha hili inatarajiwa kuongeza uzalishaji na tija, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani, kukuza ushindani, kuchochea ajira na kufungua fursa za ukuaji wa uchumi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Naybundege, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa EADB, Bernard Mono, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa taasisi hizo katika kuhamasisha na kuelekeza fedha za maendeleo kwenye sekta za uzalishaji hususani kilimo, mifugo na uvuvi kwa ujumla wake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naybundege amesema upatikanaji wa fedha nafuu ni kichocheo muhimu cha kuongeza tija, uongezaji thamani na ushindani wa biashara katika kilimo, mifugo na uvuvi.
“Hii ni sehemu ya juhudi za TADB za kufungua fursa za mitaji nafuu kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo, kuwawezesha kuongeza uzalishaji na tija, kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuimarisha ushiriki wao katika minyororo ya thamani,” amesema Naybundege.
Amesema TADB itahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa na kutumika katika shughuli zenye tija, ili kuwawezesha kufanya uwekezaji unaozingatia mzunguko wa biashara na mahitaji ya uzalishaji.
“Tunataka fedha hizi ziwe kichocheo cha uzalishaji na uongezaji thamani, Mkulima au mfanyabiashara anapopata fedha kwa masharti yanayomuwezesha kuwekeza, kuongeza uzalishaji, kusindika na kupata masoko, anaongeza thamani ya shughuli yake na kuchangia ukuaji wa uchumi wake binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EADB, Bernard Mono, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya EADB ya kupanua upatikanaji wa fedha za maendeleo na kuelekeza mitaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema kupitia ushirikiano na TADB, EADB inalenga kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wadogo kupata mitaji itakayowasaidia kuongeza uzalishaji, thamani na ushindani wa bidhaa zao, sokoni.

“Ushirikiano huu unaweka rasilimali za fedha katika maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, huku ukifungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wadogo kushiriki katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Mono.
Dirisha hilo litasaidia shughuli mbalimbali kuanzia uzalishaji hadi usindikaji, uongezaji thamani na masoko katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi. Utoaji wa fedha za muda wa kati utawawezesha walengwa kufanya uwekezaji unaohitaji muda wa kutosha kuzalisha mapato na kurejesha mikopo.
Hatua hiyo pia inatarajiwa kuchochea uwekezaji vijijini, kupunguza utegemezi wa uuzaji wa bidhaa ghafi, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa, na kuimarisha uwezo wa biashara ndogo kushiriki katika masoko yenye ushindani.
Naybundege amesema dirisha hilo maalumu linaendana na vipaumbele vya Taifa vya kujenga sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zenye tija, zinazoongeza thamani na zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na nje.

Naybundege aliishukuru EADB kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo na kupongeza timu za TADB, EADB na Serikali zilizoshiriki katika maandalizi na uanzishwaji wa bidhaa hiyo.
Amesisitza kuwa TADB kupitia dirisha hili maalum itaendelea kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kutoa matokeo chanya kwa walengwa, huku ikiimarisha ushirikiano wake na EADB katika kuchochea maendeleo ya sekta za uzalishaji, akilenga mageuzi ya kilimo.
Dirisha hili maalum la uwezeshaji la TADB-EADB la Shilingi bilioni 50 ni dhamira ya pamoja ya taasisi hizo mbili za fedha za maendeleo katika kuongeza upatikanaji wa mitaji nafuu, kuongeza tija na uongezaji thamani, na kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wadogo kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini Tanzania.



