Mambo yameiva mradi wa uondoshaji majitaka Buguruni

DAR ES SALAAM; Mradi wa uondoshaji majitaka eneo la Buguruni, Wilaya ya Ilala unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) umefikia asilimia 40, huku wakazi takribani 181,440 wakitarajiwa kunufaika na huduma hiyo pindi utakapokamilika.

‎Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Khalid Upunda, amesema ujenzi wa miundombinu ya kupokea na kusafirisha majitaka unaendelea, huku kilometa 20.2 za mtandao wa mabomba zikiwa zimelazwa kati ya kilometa 25.4 zinazotarajiwa kujengwa katika maeneo ya Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni.

‎Amesema mradi huo utahudumia wakazi wa Buguruni na maeneo mengine ya Ilala na Kinondoni, yakiwemo Mivinjeni, Mchikichini, Kariakoo, Jangwani, Gerezani, Kisutu, Mchafukoge, Upanga Mashariki, Upanga Magharibi, Kivukoni, Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni.



“Mpaka sasa tumefanikiwa kulaza mtandao wa mabomba ya kusafirisha majitaka ya inchi nane kwa umbali wa kilometa 20.2 kati ya kilometa 25.4 katika kata tatu za Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni,” amesema Upunda.

‎Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Kolon Global Corporation unatarajiwa kukamilika mwaka 2028 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 185.



‎Mhandisi Upunda ametaka wananchi kuwa wavumilivu na kushirikiana katika kulinda miundombinu itakayojengwa, akisema ushirikiano wao ni muhimu kuhakikisha mradi unakamilika na huduma inatumika kwa muda mrefu.

‎Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mivinjeni, Fadiga Mtumwa, amesema mradi huo utasaidia kupunguza changamoto ya majitaka na hatari ya magonjwa yanayohusishwa na mazingira yasiyo safi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button