Mtanzania ateuliwa CEO wa EFAfrica

ARUSHA; Mtanzania Nicomed Bohay ameteuliwa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa EFAfrica Group Ltd.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kusainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya EFAfrica, Michiel Timmerman yenye makao makuu Ebene, Mauritius, imesema Bohay atakuwa na jukumu lakuongoza utekelezaji wa mkakati wa muda mrefu wa kupanua huduma zake nchi nyingine za Afrika.
“Uteuzi huo unamweka Bohay miongoni mwa Watanzania wachache wanaoongoza taasisi za kifedha zinazofanya shughuli katika nchi nyingi za Afrika, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa mchango wa Watanzania katika uongozi wa taasisi za maendeleo ya fedha na uwekezaji barani humo,” imesema taarifa hiyo.
Bohay ana uzoefu wa takribani miaka 30 katika sekta za benki, fedha za kilimo na maendeleo ya biashara, akijikita kuongeza upatikanaji wa mali na vifaa vya uzalishaji kwa wakulima, wajasiriamali na wafanyabiashara ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.



