VETA, BGC kushirikiana kukuza ujuzi

GEITA; Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ipo katika mazungumzo na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Buckreef (BGC) ya Katoro, Geita, kwa lengo la kukuza ushirikiano utakaoandaa nguvu kazi mahiri kwa ajili ya sekta ya madini.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa kampuni hiyo Oktoba 1, 2026, Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wakufunzi na wanafunzi wa VETA pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kampuni hiyo.
”Tumezungumza na uongozi wa Buckreef kuona namna tunavyoweza kushirikiana, ikiwemo kuleta wanafunzi wetu wanaosoma fani mbalimbali ili wapate mafunzo kazini, mafunzo haya yatasaidia kukomaza ujuzi wao katika stadi wanazojifunza,” amesema Mbelle.
Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, VETA imeomba nafasi za mafunzo kwa wakufunzi wake ili waweze kupata ujuzi mpya na kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Aidha, Mbelle amesema VETA itashirikiana na Buckreef kuhakikisha wananchi wanaozunguka mgodi huo wanapata mafunzo ya ufundi stadi yatakayofadhiliwa na kampuni hiyo.

”Buckreef wameona kuwa sisi VETA tunaweza kutoa ujuzi kwa vijana wa maeneo haya, na sisi tumeona jinsi tutakavyoandaa programu za kuwawezesha vijana wanaozunguka eneo la mgodi kupata ujuzi katika stadi mbalimbali,” amefafanua.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa mgodi huo, Isaac Bisansaba, amewataka wananchi wanaozunguka mgodi huo kujiandaa kunufaika na fursa zitakazotokana na ushirikiano huo.

”Tayari tumeanza mchakato wa kuwatambua vijana waliomaliza kidato cha sita, kidato cha nne au hata wale ambao hawakufaulu kwa viwango vya juu, ili tuwasaidie kujiunga na vyuo vya VETA kwa kulipia sehemu ya gharama za mafunzo yao na baadaye kuwapa nafasi za mafunzo kwa vitendo mgodini kwetu,” amesema Bisansaba.



