Kilimo, mifugo na uvuvi watakiwa kuongeza tija kufikia Dola bilioni 100

SEKTA za Kilimo, Mifugo na Uvuvi zimetakiwa kuongeza uzalishaji, kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuboresha tija ili kuchangia Dola za Marekani bilioni 100 katika uchumi wa Tanzania kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Lengo hilo ni sehemu ya mkakati wa Tanzania kuelekea uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja, ambapo sekta za uzalishaji zimepewa nafasi kubwa katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Barani Afrika, yanayoambatana na Maonesho ya Tatu ya Kilimo, Mifugo na Ufugaji wa Kuku Barani Afrika, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Wizara ya Mifugo, Stephen Michael, amesema kuongeza tija katika sekta hizo ni muhimu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Michael, aliyemwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Ally Kakurwa, amesema uwekezaji katika teknolojia za kisasa na kuongeza uzalishaji utaiwezesha Tanzania kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula, sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. SOMA: Matumizi mbegu bora yafika Malagosi, Mgama, Magulilwa
Amesema sekta za mifugo na uvuvi zina nafasi kubwa katika kuongeza pato la taifa na kupata fedha za kigeni, hususan kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye ushindani na zinazoweza kuuzwa katika masoko ya ndani na kimataifa.
“Sekta ya mifugo na uvuvi zina jukumu kubwa la kutimiza hayo, kwa kuwa zitasaidia kuongeza usalama wa chakula, ajira kwa Watanzania, pato la taifa pamoja na fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi,” amesema Michael.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazalishaji, wawekezaji na wadau mbalimbali katika sekta hizo ili kuongeza uzalishaji, kutumia teknolojia bora na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata masoko ya uhakika. Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, kukuza biashara na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na fursa zilizopo katika masoko ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Michael, utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 unahitaji sekta za uzalishaji kupewa msukumo zaidi kupitia teknolojia, uwekezaji na upatikanaji wa masoko, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.



