Wawekezaji wavutiwa sekta ya kilimo

TANZANIA imeendelea kujijenga kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na fursa kubwa zilizopo katika sekta ya kilimo, huku wawekezaji kutoka India, Ulaya na Mashariki ya Kati wakionesha nia ya kuwekeza nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAB Group, Tahir Bari, amesema wawekezaji hao tayari wameanza kufanya mazungumzo na mamlaka za Tanzania kuhusu mazingira ya uwekezaji, taratibu za upatikanaji wa leseni na mahitaji muhimu kabla ya kuanzisha shughuli zao nchini.
Bari amesema hayo Septemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Barani Afrika, yaliyoambatana na Maonesho ya Tatu ya Kilimo, Mifugo na Ufugaji wa Kuku yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Saba Saba.
Amesema Tanzania imekuwa sehemu ya mipango ya TAB Group kwa muda mrefu, jambo lililowasukuma kuandaa maonesho hayo nchini kwa lengo la kuwaunganisha wadau wa kilimo, wafanyabiashara, wawekezaji na kampuni za kimataifa.
Kwa mujibu wa Bari, uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya kilimo unaweza kuongeza uhamishaji wa teknolojia na maarifa, hasa kwa wakulima wadogo, na kusaidia kuongeza tija pamoja na thamani ya bidhaa za kilimo. Amesema Tanzania pia inaweza kujifunza kutoka India katika kuendeleza kilimo, kutokana na hatua kubwa ambayo nchi hiyo imepiga katika kipindi cha miaka 40 hadi 50 iliyopita.
Bari amesema baadhi ya mazingira ya uzalishaji kati ya Tanzania na India yanafanana, ikiwemo ukubwa wa mashamba, hivyo uzoefu wa India unaweza kusaidia kutengeneza teknolojia na suluhisho zinazowalenga zaidi wakulima wadogo.
Aidha, ameipongeza Serikali na taasisi mbalimbali kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wawekezaji wa kimataifa, akisema hatua hiyo inasaidia kuwawezesha wawekezaji kuelewa fursa na taratibu za kuanzisha shughuli zao nchini.SOMA: Kilimo, mifugo na uvuvi watakiwa kuongeza tija kufikia Dola bilioni 100



