Polisi wanawake Arusha wakumbushwa uadilifu

ARUSHA: KAMANDA wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amewataka askari wa kike wa Jeshi la Polisi mkoani humo kuwa waadilifu katika utumishi wa umma na kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria na kulinda raia pamoja na mali zao, kwa lengo la kujenga imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Ngailo aliyasema hayo jana usiku akiwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net Gala) Mkoa wa Arusha, yaliyokwenda sambamba na hafla ya kuwaaga askari 10 wa kike waliostaafu.

Alisema Jeshi la Polisi ni taasisi muhimu katika utekelezaji wa sheria na ulinzi wa raia pamoja na mali zao, hivyo uadilifu wa askari ni msingi muhimu wa kujenga na kulinda imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

“Rushwa inapojitokeza katika utoaji wa huduma za umma huathiri haki, usawa na imani ya wananchi kwa Serikali na taasisi zake,” alisema.

Ngailo alisema kila mtumishi ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma.

Aliwataka Polisi wanawake kutumia nafasi zao kuwa mabalozi wa uadilifu, kupinga vitendo vya rushwa na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa maadili.

Alisema kutokana na kuwa karibu na wananchi na kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiusalama na kijamii katika mhimili wa haki jinai, Polisi wanawake wana nafasi muhimu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya rushwa, ikiwemo rushwa ya ngono, pamoja na kuhamasisha wananchi kukataa vitendo hivyo na kutoa taarifa vinapotokea.

Aidha, Ngailo aliwapongeza askari wanawake waliostaafu kwa kutimiza wajibu wao wa kulitumikia Taifa kupitia Jeshi la Polisi, akisema wametumia muda, nguvu, maarifa na utaalamu wao kujenga na kulinda nchi.

“Mmetumia muda, nguvu, maarifa na utaalamu wenu kulitumikia Taifa kupitia Jeshi la Polisi. Mnapomaliza utumishi wenu, ni wazi mnaenda kuanza sehemu nyingine muhimu sana katika maisha yenu mkiwa nje ya utumishi wa moja kwa moja wa Jeshi la Polisi. Kwa dhati, mchango wenu hautasahaulika katika utumishi wa umma,” alisema.

Ngailo pia aliipongeza TPF Net Mkoa wa Arusha kwa kuandaa maadhimisho hayo, akisema yamegusa maeneo muhimu yenye tija katika kuwaelimisha, kuwashauri na kuwasaidia askari wanawake.

Aliwahimiza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, weledi, uadilifu na uzalendo, akisisitiza kuwa uadilifu wa mtu mmoja una heshima ya Jeshi zima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPF Net Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Lukololo, alisema mtandao huo una jumla ya askari wanawake 547 mkoani Arusha.

Alisema lengo la mtandao huo ni kuwawezesha na kuwaelimisha askari wanawake, hususan kuhusu masuala ya kisheria, ili waweze kuwa watumishi bora katika utekelezaji wa majukumu yao.

Lukololo alisema maadhimisho hayo yalianza Septemba 1 hadi 4, 2026, huku kilele chake kikifanyika Septemba 5 na kwenda sambamba na kuwaaga askari wenzao 10 waliostaafu.

Alisema katika kipindi cha maadhimisho hayo, askari wanawake walipata elimu mbalimbali, ikiwemo kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, matendo ya huruma, afya, huduma bora na uongozi bora.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button