Tanzania, India mpango mpya kuendeleza kilimo

DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India imeanza kuchukua hatua mahsusi za kuendeleza sekta ya kilimo, ikiwemo kuandaa majukwaa yatakayounganisha wadau wa sekta hiyo na kuwawezesha kujifunza, kujenga mitandao ya mahusiano pamoja na kuingia katika ubia wa kibiashara.
Hayo yamesemwa leo, Septemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TAB Group, Tahir Bari, wakati wa Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Barani Afrika, yaliyoambatana na Maonesho ya Tatu ya Kilimo, Mifugo na Ufugaji Kuku Barani Afrika, yaliyowakutanisha zaidi ya kampuni 1,000 kutoka katika nchi 35, yakilenga kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya kilimo kubadilishana ujuzi, teknolojia na fursa za uwekezaji na biashara.
Bari amesema amevutiwa na ushiriki mkubwa wa vijana katika maonesho hayo, huku akieleza kuwa vijana wengi wameanza kuitazama kilimo kama biashara na wanaonyesha utayari wa kujifunza na kuchunguza fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Amesema mabadiliko hayo yanaonyesha umuhimu wa kuondokana na dhana kwamba kilimo ni shughuli inayofaa kwa wazee pekee, akisisitiza kuwa vijana wanaweza kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali kuongeza tija na kuboresha uendeshaji wa shughuli za kilimo.
Aidha, amesema teknolojia zinazopatikana kwa sasa hazihitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, kwani kuna mifumo iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya wakulima wenye mashamba madogo.
Kwa mujibu wa Bari, amesema upatikanaji wa teknolojia hizo unatoa fursa kwa vijana kuingia katika kilimo kwa kutumia mifumo wanayoweza kumudu kifedha, huku wakinufaika na taarifa, maarifa na zana za kidijitali zinazoweza kusaidia katika uzalishaji na biashara.
Amesema matumizi ya teknolojia, pamoja na majukwaa yanayowaunganisha wadau wa sekta hiyo, yanaweza kuwa kichocheo muhimu katika kuwavutia vijana zaidi kwenye kilimo na kukifanya kuwa sekta yenye ushindani na fursa kubwa za biashara.



