JNHPP kuipa Tanzania nafasi mpya biashara za kikanda

PWANI: Serikali inalenga kutumia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ( JNHPP) kuongeza uzalishaji wa umeme na kuiweka Tanzania katika nafasi muhimu ya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi huo umejengwa katika eneo la Mto Rufiji na umebuniwa kuwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme.

Twange amesema jumla ya mitambo hiyo tisa imebuniwa kuzalisha megawati 2,115, hatua ambayo itaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania katika uzalishaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara.

Amesema Serikali kupitia TANESCO ilisaini mkataba wa ujenzi wa mradi huo tarehe 12 Desemba 2018 na kampuni za Arab Contractors na Elsewedy Electric, zote kutoka Misri, huku siku moja kabla, tarehe 11 Desemba 2018, Serikali ikimkabidhi TANESCO jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, amesema tarehe 17 Aprili 2019 TANESCO ilisaini mkataba na TANROADS kwa ajili ya masuala ya ushauri na usimamizi wa baadhi ya shughuli za mradi.

Kwa mujibu wa Twange, Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi mkubwa wa kihandisi wenye miundombinu ya kisasa na ya kimkakati, ukiwa na vipengele sita muhimu vinavyounda kituo hicho cha kuzalisha umeme.

Ameeleza kuwa bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji takribani mita za ujazo bilioni 32.784, huku maji yanayoingia kwenye bwawa yakitokana na vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni Mto Kilombero unaochangia asilimia 65, Mto Luwegu asilimia 19 na Mto Ruaha asilimia 15.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button