Mwang’oda aagiza usimamizi miradi ya CSR

GEITA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda, ameagiza viongozi wa serikali kushiriki, kufuatilia na kusimamia kikamirifu miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).
Mwang’oda ametoa maagizo hayo alipoongoza msafara wa mbio za mwenge kutembelea, kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Lwamugasa wilayani Geita.
Amesema fedha za CSR zinazotolewa na makampuni ni fedha halali za watanzania kwa kuwa zinatolewa kwa mjibu wa sheria za nchi na hivo miradi ushiriki wa viongozi wa serikali ni jambo muhimu.

“CSR inatolewa kwa mjibu wa sheria, kwa ajili ya kurudisha kwa wananchi, kwa kuwa wanarudisha kwa jamii, basi serikali isimamie kwa ukaribu, tusiwaachie wadau wetu wa maendeleo peke yao”, amesema.
Aidha, ameagiza kituo cha afya Lwamugasa kuunganishiwa umeme ili kuruhusu miundombinu iliyojengwa na serikali kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi kusudiwa wa eneo la Lwamugasa.
Amesema haina afya kuona ujenzi wa miundombinu yote umekamilika, vifaa tiba vimenunuliwa na watoa huduma za afya wameajiliwa lakini kituo cha afya hakitoshelezi kutoa huduma kwa kukosa umeme.

“Kitakwimu kata hii ina zaidi ya wananchi elfu 72, niombe wanaohusika waweze kuleta umeme mahala hapa ili huduma zingine zianze kutolewa katika kituo hiki”, amesema.
Naibu Waziri wa Tamisemi na Mbunge wa Jimbo la Busanda, Dk Jafari Rajabu Self amesema kituo cha afya Lwamugasa kinatarajia kuhudumia takribani wananchi 72,000 wa kata ya Lwamugasa.
“Kati ya wananchi hao elfu 72, wapo kina mama wanaojifungua kwa mwezi, wastani wa kina mama 250 na Lwamugasa hapakuwa kabisa na kituo cha afya.
Awali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Lwamugasa, Charles Anthony amesema mradi umegharimu takribani sh bilioni 1.24 kati yake sh milioni 565 ni fedha za CSR kutoka kampuni ya Bucreef.



