Mwang’onda azitaka halmashauri Kigoma kuvutia wawekezaji

KIGOMA: Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Wazo Mwang’onda, amezitaka halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Mwang’onda alitoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Kituo cha Mafuta cha Remmy, kilichopo Kijiji cha Nyachenda, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, ambacho kinajengwa na mwekezaji binafsi kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 500.
Alisema uwekezaji binafsi ni sehemu muhimu ya jitihada za kuharakisha maendeleo nchini, hivyo halmashauri zinapaswa kushirikiana na wawekezaji kwa kuweka mazingira yatakayowezesha miradi yenye tija kutekelezwa katika maeneo yao.

Mwang’onda alisema hatua za kuondoa vikwazo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi zimeongeza fursa za uwekezaji, hivyo ni muhimu halmashauri kutumia fursa hizo kuvutia miradi inayoweza kuongeza shughuli za kiuchumi na manufaa kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa amani na usalama katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa salama, akisema hali hiyo ni muhimu katika kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.

Awali, Meneja wa Kituo hicho cha Mafuta, Neema Razaro, alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh milioni 518 hadi kukamilika, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Razaro alisema mradi huo umefanikiwa kutokana na ushirikiano walioupata kutoka Serikali ya Wilaya ya Kasulu, hali iliyowawezesha wawekezaji wa ndani kuutekeleza.

Alisema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa sehemu ya kuongeza huduma na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, sambamba na kuchangia jitihada za Serikali za kuweka mazingira yatakayowezesha uwekezaji na maendeleo ya wananchi.



