Wanandoa watakiwa kuheshimiana, kuaminiana

DAR ES SALAAM: Wanandoa wametakiwa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kuaminiana, kuheshimiana na kushirikiana katika masuala ya kifamilia na kiuchumi ili kuimarisha ndoa na kujenga familia zenye mshikamano.

Wito huo umetolewa katika hafla ya Wanandoa (Couples Night) iliyoandaliwa na PIMEA, jukwaa linalolenga kusaidia wanandoa kujenga upya, kurejesha na kuimarisha ndoa zao kupitia mafundisho ya kibiblia pamoja na hekima ya vitendo.

Akizungumza katika hafla hiyo, msanii wa muziki wa Injili, mwanzilishi na mwenyeji wa Usiku wa Wanandoa,  Dk Christine  Mbelwa, amesema ndoa ni msingi muhimu wa familia na jamii, hivyo wanandoa wanapaswa kuwa tayari kujifunza na kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha ya ndoa.

Amesema uwazi ni muhimu katika ndoa, hususan katika masuala ya uchumi wa familia, akiwataka wanandoa kuepuka kufichana mambo yanayoweza kuathiri uhusiano wao.

“Tunawahimiza wanandoa kusikilizana, kuaminiana na kushirikiana. Hata katika masuala ya kiuchumi, ni muhimu kuwa wawazi na kufanya maamuzi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi wa familia,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mbelwa, PIMEA imekuwa ikitoa mafundisho na mafunzo ya vitendo yanayowasaidia wanandoa kuelewa namna ya kutumia kanuni za kibiblia na hekima katika kujenga, kuendesha na kudumisha ndoa zenye mafanikio.

Amesema tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, wameendelea kushuhudia wanandoa wakijenga upya mahusiano yao, kurejesha mshikamano na kuimarisha ndoa zao kupitia elimu na matumizi ya kanuni hizo.

“Ndoa imara huchangia familia imara; familia imara huchangia jamii imara na jamii imara hujenga taifa lenye nguvu na ustawi,” amesema.

Dk Mbelwa amewataka wanandoa kuendelea kujaliana na kutunzana, huku wakitafuta suluhisho la changamoto zao kwa njia ya mazungumzo badala ya kuruhusu migogoro ivunje mshikamano wao.

“Ndoa yako inaweza kuwa bora zaidi. Jifunze, shiriki na weka katika vitendo mambo unayojifunza ili kuona mabadiliko katika ndoa yako,” amesema.

Aidha, amewahimiza wanandoa kushiriki katika matukio yajayo ya Couples Night ili kupata maarifa na mbinu zinazoweza kuwasaidia kuimarisha uhusiano wao na kujenga familia zenye amani.

 

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button