Programu ya AFDP yawafikia wakulima Tanga

TANGA: UJUMBE kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) pamoja na wataalamu kutoka sekta mbalimbali zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) wamewasili Mkoani Tanga kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa programu hiyo.
Timu hiyo ilifanya ziara hiyo Septemba 7, 2026 kwa lengo la kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kupitia AFDP, sambamba na kubaini mafanikio na changamoto zilizopo katika maeneo husika.
Katika ziara hiyo, timu hiyo itatembelea maeneo yanayotekeleza programu katika Mkoa wa Tanga.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, timu itatembelea Kata ya Msomela iliyopo katika Halmashauri ya Handeni Vijijini, ambako programu imewezesha jamii ya Kimasai, ambayo kwa asili ni wafugaji, kuanza kujihusisha na kilimo chenye tija hususan cha zao la mahindi.
Kupitia programu hiyo, wakulima wamepatiwa elimu ya kilimo bora na kuanzishwa kwa mashamba darasa (FFS) kwa ajili ya mazao ya alizeti, mahindi na maharage. Mashamba hayo yameonesha mafanikio makubwa ambapo hekta moja imekuwa na uwezo wa kuzalisha takribani magunia 20 yenye uzito wa kilo 100 kila moja.
Hatua hiyo imewezesha jamii ya wafugaji kuongeza shughuli za uzalishaji wa chakula na kunufaika na mazao yanayolimwa, hivyo kuchangia kuboresha maisha yao.

Kwa upande wa sekta ya uvuvi, Programu ya AFDP inaendelea na ujenzi wa Soko la Kimataifa la Samaki Kipumbwi lililopo katika Halmashauri ya Pangani. Ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 68 na linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.

Aidha, programu hiyo inaendelea na ujenzi wa vichanja 40 vya kukaushia dagaa ambavyo vina uwezo wa kukausha takribani tani tano za dagaa kwa wakati mmoja.
Vilevile, AFDP inaendelea na ujenzi wa ghala la baridi pamoja na mtambo wa barafu katika soko hilo kwa ajili ya kuhifadhi na kuwezesha usafirishaji wa samaki kwa ubora unaohitajika.

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini Tanzania, Seth Meng, alikutana na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Emmanuel Kisongo, na kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa programu hiyo pamoja na mafanikio yanayotarajiwa kwa wananchi wa maeneo yanayotekelezwa miradi hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga alieleza kuwa programu hiyo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta za kilimo na uvuvi mkoani humo.

Alitoa shukrani kwa IFAD kwa kuendelea kuwafikia wananchi wa Mkoa wa Tanga na kuomba, ikiwezekana, uwekezaji zaidi uongezwe ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.



