Wakulima waliokata tamaa Wasa wapewa elimu ya mbegu bora

IRINGA: KILIO cha muda mrefu cha wakulima wa kata ya Wasa wilayani Iringa, kuhusu kuuziwa mbegu feki na watu wasio waaminifu kimepata suluhu kufuatia elimu juu ya matumizi ya mbegu bora na njia za kuzipata.

Elimu hiyo imefika vijijini siku chache baada ya wananchi wa kata hiyo kumweleza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamini Sitta, namna mbegu zisizo na ubora zinavyowakatisha tamaa, kupunguza uzalishaji na kuwaongezea hasara kila msimu wa kilimo.

Katika mikutano iliyofanyika katika vijiji mbalimbali vya kata hiyo na kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds ambaye pia ni wakala wa Mbegu za Kilimo za Serikali (ASA), wakulima wameelekezwa umuhimu wa kutumia mbegu zinazokidhi viwango, kufuata kanuni bora za kilimo na kuwa makini na watu wanaosambaza mbegu bila uhalali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihomasa, Yohakimu Mgao, amesema wakulima wanahitaji mbegu bora; wanataka mnyororo mzima wa uzalishaji na masoko uboreshwe ili juhudi zao ziwe na tija.

“Tunataka magari makubwa ya tani 10 na kuendelea yaanze kuja katika vijiji vyetu kubeba mizigo toka mashambani. Tukizalisha kwa wingi, tunahitaji pia kuwa na uhakika wa namna ya kuyafikisha mazao yetu sokoni,” amesema Mgao.

Amesema ziara ya hivikaribuni ya Mkuu wa Wilaya ilitoa fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao, ikiwamo suala la mbegu feki, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wakulima.

“Tumefikisha malalamiko yetu na sasa tunaona hatua zikianza kuchukuliwa. Tunataka mkulima apate mbegu yenye uhakika na awe na matumaini ya kupata mavuno mazuri,” amesema.

Mtendaji wa Kata ya Wasa, Maisha Magava, amesema matumizi ya pembejeo sahihi ni sehemu muhimu ya safari ya mkulima kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo chenye tija na kinachoweza kuongeza kipato cha kaya.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Wasa, Erasto Fundo, amesisitiza umuhimu wa wakulima kutambua aina ya mbegu akisema mkulima anapaswa kuzingatia ubora wa mbegu, na mazingira ya eneo ili kuongeza uwezekano wa kupata mavuno bora.

Mkurugenzi wa Mgongolwa Agrovet and Seeds na Wakala Mkuu wa Mbegu za Serikali (ASA), Joseph Mgongolwa, amesema hatua ya kuwafikia wakulima vijijini inalenga kuhakikisha elimu na mbegu bora vinawafikia walengwa moja kwa moja.

Mgongolwa amewataka wakulima kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaotumia mwanya wa mahitaji ya pembejeo kuuza mbegu zisizo na ubora.

“Uonevu kwa wakulima ufike mwisho. Kamateni vishoka wanaouza mbegu feki kwa wakulima. Chama na Serikali visichukiwe kwa sababu ya wahuni wachache wanaohujumu juhudi na matamanio ya wananchi,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button