Chikota azungumzia faida kongani ya viwanda Maranje

MTWARA: MBUNGE wa Jimbo la Nanyamba Mkoani Mtwara Abdallah Chikota amesema uwepo wa ujenzi wa kongani ya viwanda ya korosho iliyopo kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara ni faida kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo hasa suala la ajira kwa vijana.
Hayo yamejiri leo Septemba 7,2026 wakati mbunge wa jimbo hilo alipotembelea kwenye jimbo hilo na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali kupitia mikutano ya hadhara.

Aidha vijiji hivyo ikiwemo cha tulia, maranje, mkuranga, malamba, maili, mtiniko na vingine lengo likiwa kuwashukuru na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo kufuatia ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu uliyofanyika Oktoba 29, 2025.
Pia kujionea na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao ili ziweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo ikiwemo ya maji, barabara, umeme, afya na zingine sambamba na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo kwenye maeneo hayo ikiwemo mabati na saruji.

Aidha kata hiyo ya mtiniko ni ya kwanza kwa mbunge huyo kuanza rasmi ziara hiyo ya siku tano kwenye jimbo hilo kati ya kata 17 zilizopo kwenye halmashauri hiyo.
Amesema ili kukabiliana na changamoto ya zao la korosho wananchi wa maeneo hayo wamepata bahati ya kujengewa kongani hiyo.
Aidha ujenzi huo wa kongani bado unaendelea na makampuni mengi yanaomba nafasi ya kuja kuwekeza kwenye kiwanda hicho hivyo ni fursa kubwa kwao.
Mbali na hilo amewashukuru wananchi hao wa kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa kura nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, mbunge huyo na viongozi wengine kwa ujumla katika jimbo hilo.
“Ndugu zangu niwape matumaini kwa kukichagua chama cha mapinduzi hamjapoteza kwahiyo niwashukuru sana wananchi kwa kukichagua chama cha mapinduzi”amesema Chikota
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mtwara Vijijini Nashir Mfaume
amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa, uchaguzi umeshapita hivyo sasa ni wakati wa kushirikiana na uongozi wa kata hiyo na halmashauri kwa ujumla ili kujiletea maendeleo.
Baadhi ya wananchi hao akiwemo Kaisi Mussa mkazi wa kijiji cha tulia ameishukuru serikali kwa kuwaletea ujenzi huo ambao unaenda kuleta fursa ya ajiira kwa vijana.
Hata hivyo Hamza Hassan mkazi wa kijiji hicho ameuomba uongozi wa halmashauri hiyo kusimamia suala la malipo ili yatoke kwa wakati kwa baadhi ya vijana wanaopata ajira kwenye kongani hiyo kutokana kuna kipindi huwa hayatoki kwa wakati



