Aliyejifungua watoto 3 akumbukwa, msaada zaidi wahitajika

DODOMA; Msamaria mwema ametoa msaada wa chakula na mahitaji mengine ya nyumbani kwa mama wa watoto tisa anayeishi Kijiji cha Igamba, Kata ya Dabaro, wilayani Chamwino, Dodoma anayepitia magumu ya kulea familia ya watoto tisa peke yake, wakiwemo watoto watatu pacha.

Julai, mwaka huu, magazeti ya Daily News, HabariLEO pamoja na mitandao ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), iliripoti changamoto anazopitia mama huyo, Rehema Mnyodo, tangu alipojifungua watoto watatu katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino takribani miaka miwili iliyopita, huku mumewe akitumikia kifungo jela.

Msaada huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na msamaria huyo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa, katika tukio lililoshuhudiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igamba, Elias Wami, pamoja na wanafamilia wa mnufaika.

Hata hivyo, Rehema hakuwepo kwenye tukio hilo baada ya kulazimika kumkimbiza mmoja wa pacha hao katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino kufuatia matatizo ya kiafya.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igamba, Elias Wami alimshukuru mfadhili huyo kwa kuguswa na mazingira magumu anayopitia mwanamke huyo, akieleza kuwa mume wake bado anatumikia kifungo katika Gereza la Isanga mkoani Dodoma.

Wami pia alitoa wito kwa wasamaria wema wengine kujitokeza kumsaidia mama huyo anayepambana kujikimu kimaisha hasa ikizingatiwa watoto wake wameshindwa kwenda shule licha ya kutimiza umri wa kuanza safari ya kielimu.

Mama huyo, ambaye pia anawalea pacha hao wenye umri wa miaka miwili, anategemea vibarua ili kuishi, jambo linalomwia vigumu kupata hata mahitaji ya msingi ya familia.

Ugumu wa maisha umewalazimisha watoto wake wenye umri wa kwenda shule kubaki nyumbani, ingawa serikali inatoa elimu bila malipo.

Kila anapopata kibarua cha muda, watoto wake wakubwa hubaki nyumbani kuwazoea wadogo zao badala ya kwenda shuleni.

Wakati gazeti la Daily News lilipotembelea hifadhi yake ya muda, binti yake mmoja mwenye umri wa miaka 11 alikuwa akiwalea pacha hao, huku binti yake mwingine aliye na ujauzito naye akiwa anategemea msaada kutoka kwa Rehema.

Mwanamke huyo aliiambia Daily News hivi karibuni kuwa hali yake ilizorota zaidi baada ya kulazimika kuondoka katika nyumba ya familia kufuatia kufungwa jela kwa mume wake.

Kulingana naye, kwa sasa anaishi kwenye nyumba ya ndugu yake na anahofia kuondolewa pindi mwenye nyumba atakaporudi kutoka Dar es Salaam.

Kisa cha Rehema kinaonesha jinsi umaskini uliokithiri unavyoendelea kuwanyima baadhi ya watoto haki ya kupata elimu, kujapokuwa na sera ya elimu bila malipo.

Pia kinasisitiza haja ya familia zilizo katika mazingira hatarishi kubainishwa na kujumuishwa kwenye programu za hifadhi ya jamii kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Kwa Rehema, msaada wowote hautakuwa tu wa chakula na hifadhi, bali pia utatoa fursa kwa watoto wake kurejea darasani na kujenga maisha ya baadaye yaliyo bora.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Igamba, Loveness Kimambo, alisema Rehema ameingizwa kwenye Mradi wa Mbuzi wa shirika la Save the Children, ambao unatoa maziwa kwa mama wanaonyonyesha.

Hata hivyo, alisema msaada huo hautoshi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya familia hiyo.

“Wakati mwingine tumekuwa tukihamasisha michango ya chakula kutoka kwa wanakijiji, lakini familia hii inahitaji msaada mkubwa zaidi wa haraka, hasa ili kuwezesha watoto hawa kwenda shule,” alisema Kimambo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button