Wataka taekwondo itumike kuhamasisha amani

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Taekwondo Tanzania limewataka viongozi, wanamichezo na wadau wa mchezo huo kuendelea kushirikiana na kutumia Taekwondo kuhamasisha amani, umoja na nidhamu kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika mashindano ya saba ya Korean Ambassador Cup yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Abdallah Ally, amesema michezo ina nafasi kubwa katika kuunganisha watu na kujenga jamii yenye mshikamano.
“Napenda kusisitiza kuhusu amani, umoja na nidhamu. Tunataka kufanya vizuri kwa ajili ya binadamu na kwa ajili ya maendeleo ya mchezo wetu. Kwa hiyo, kupitia uongozi huu na wadau wote, tunapaswa kuwa wamoja na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye utulivu, upendo na amani,” amesema.
Ally amesema amani ni sehemu muhimu ya maisha ya Watanzania, hivyo taekwondo inapaswa kuendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha amani nchini na duniani kupitia shughuli mbalimbali za mchezo huo.
Amesema mashindano ya Korean Ambassador Cup, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na Ubalozi wa Korea, ni miongoni mwa majukwaa yanayowaunganisha wanamichezo kutoka maeneo mbalimbali na kutoa nafasi ya kujenga urafiki na uhusiano kupitia Taekwondo.

Kwa upande wake, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Petro Gallus, amesema Serikali inaunga mkono jitihada za kukuza Taekwondo na kuhakikisha mashindano yanaendeshwa katika mazingira salama kwa kuzingatia sheria na taratibu za mchezo.
Gallus amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Korea kupitia taekwondo unasaidia kukuza vipaji vya Watanzania na kuufanya mchezo huo kufahamika zaidi, hasa kwa kuwa bado haujaenea kwa kiwango sawa na baadhi ya michezo mingine nchini.
Katibu wa Pili na Balozi Mshauri wa Ubalozi wa Korea nchini Tanzania, Seonggyeong Kim, amesema Taekwondo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Korea, ambako watu wengi huanza kujifunza mchezo huo wakiwa wadogo.

Kim amesema Taekwondo hujenga mwili na akili, huwafundisha vijana uvumilivu, nidhamu na uwezo wa kujitawala, maadili ambayo amesema ni muhimu katika kujenga kizazi bora.
Amesema anaamini kuwa Watanzania wengi wanaopenda taekwondo wataendelea kupata fursa ya kujiunga na kufanya mazoezi ya mchezo huo, huku akisisitiza kuwa licha ya umbali wa kijiografia kati ya Korea na Tanzania, taekwondo imekuwa daraja la kuziunganisha nchi hizo.



