‘Wagonjwa wa ubongo, uti wa mgongo wapatiwe ushauri wa kitaalamu’

Dar es Salaam: Takribani watu 70 wenye changamoto mbalimbali zinazohusiana na ubongo na uti wa mgongo wamepatiwa ushauri wa kibingwa na Daktari Bingwa na Mbobezi wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, kutoka Hospitali ya Medanta ya Gurugram nchini India, Dk Karanjit Singh.
Dk Singh amekutana na wagonjwa hao jijini Dar es Salaam, ambapo ametoa ushauri kuhusu namna sahihi ya kupata matibabu kwa changamoto zao, akisisitiza kuwa baadhi ya matatizo hayo yanaweza kutibiwa bila mgonjwa kufanyiwa upasuaji.
Amesema ni muhimu wagonjwa kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanyiwa upasuaji, ili kuepuka kufanyiwa matibabu ambayo huenda yasiwe ya lazima na yanayoweza kuongeza changamoto wanazokabiliana nazo.
Kwa upande wake, daktari kutoka Hospitali ya Tiba ya Jioni ya Dar es Salaam, Dk Mustafa Dadam, amesema ujio wa Dk Singh nchini Tanzania ni mara ya tatu mwaka huu, ukiwa na lengo la kusaidia Watanzania kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu njia sahihi za matibabu ya magonjwa ya ubongo na uti wa mgongo.
Dk Mustafa amesema baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakilazimika kufanyiwa upasuaji kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kushindwa kumudu gharama za kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kupata ushauri na matibabu kutoka wataalamu bingwa.
-Amesema uwepo wa madaktari bingwa kutoka nje ya nchi nchini Tanzania unatoa fursa kwa familia ambazo hazina uwezo wa kusafiri kwenda nje ya nchi kupata ushauri wa kitaalamu na sahihi kuhusu changamoto zinazowakabili wagonjwa wao.
Dk Mustafa ametaja baadhi ya dalili zinazoweza kuashiria matatizo yanayohusiana na ubongo na uti wa mgongo kuwa ni maumivu ya mgongo yanayoshuka hadi miguuni, maumivu ya shingo yanayosambaa hadi kwenye mabega au mikono, kupata ganzi, udhaifu wa mwili pamoja na maumivu ya kichwa ya muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Medicredi, Latifa Chauhan, amesema zoezi hilo lililofanywa chini ya usimamizi wa Dk Singh limekuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa na Watanzania kwa ujumla, kwa kuwapatia fursa ya kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu bingwa bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.



