Mbunge ACT Wazalendo amsifu Rais Samia miradi Kigoma

KIGOMA; MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa Chama cha ACT Wazalendo Kiza Nayeye amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa kwenye jimbo lake, ambayo anasema imeondoa changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili.
Mayeye amesema hayo wakati Mwenge wa Uhuru ukiweka mawe ya msingi katika miradi ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Msimba Day na madaraja 16 ya mawe, miradi ambayo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi hao na kikwazo katika mipango yao mbalimbali ya maendeleo.
Amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo ilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa kata hiyo, ambao walilazimika kutembea umbali mrefu hadi Sekondari ya Mwandiga.

Kufuatia ujenzi wa shule hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wazo Mwang’onda alitoa rai kwa wazazi kutumia utekelezwaji wa mradi huo kama jambo la thamani kwao kuhakikisha watoto wao wanaenda shule, wanazingatia masomo, lakini pia kuhakikishaa miradi hiyo inalindwa na kutunzwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya Kigoma, Chiriku Chilumba alisema shule hiyo itakayogharimu kiasi cha Sh milioni 603 ni moja ya shule mbili zilizojengwa, ili kusogeza huduma karibu na wananchi, lakini pia kujiandaa na ongezeko la wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka ujao.



