IJA yawapiga msasa madalali wa mahakama

DAR ES SALAAM; Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kimeanza mafunzo ya kundi la 17 ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama, yakilenga kuwajengea uwezo washiriki 30 kutoka mikoa mbalimbali nchini kutekeleza amri za mahakama kwa ufanisi, weledi na uadilifu, hivyo kuchangia upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Akifungua mafunzo hayo ya wiki mbili leo Septemba 14, 2026 jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi na Rushwa,  Sharmillah Sarwatt, amesema kila jukumu linalotekelezwa na madalali wa mahakama linapaswa kufanywa kwa weledi kwa kuwa linaweza kugusa uhuru na haki za mtu, na kutotekelezwa ipasavyo kunaweza kusababisha malalamiko na kuvuruga amani.

Sarwatt pia amewakumbusha washiriki kuhusu hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, aliyoitoa Juni 30, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama jijini Dodoma, ambapo aliwatambua madalali hao kuwa wadau na nguzo muhimu katika mchakato wa utoaji haki, kwa kuwa utekelezaji wa maamuzi ya mahakama unategemea kwa kiasi kikubwa kazi yao.

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri wa IJA,  Fatuma Mgomba, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa kuzingatia zaidi vitendo, ili kuwezesha washiriki kupata ujuzi na umahiri wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mafunzo hayo yatakayofanyika hadi Septemba 30, 2026 na washiriki watafanya mitihani ya umahiri na watakaofaulu watapatiwa vyeti vitakavyowawezesha kuomba na kufanya kazi za mahakama, pamoja na kufanya minada katika taasisi za serikali na sekta binafsi, ikiwemo benki na mashirika ya fedha.

 

IJA imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na 6 za Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na. 363 za mwaka 2017, kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wenye nia ya kufanya kazi hiyo na kuboresha mnyororo wa utoaji haki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button