‘Sekta ya uvuvi inahitaji uwezeshaji wa kifedha mbadala’

DAR ES SALAAM: UWEZESHAJI kifedha sekta ya uvuvi unahitaji suluhisho bunifu zaidi ya mikopo ya kawaida ya benki ili kukidhi mahitaji na changamoto za kipekee zinazowakabili wavuvi, wafugaji wa samaki, wafanyabiashara, wachakataji na wadau wengine katika mnyororo wa thamani, wataalamu wamesema.

Wamesema taasisi za fedha zinapaswa kuzingatia aina mbalimbali za huduma za kifedha, ikiwemo mikopo inayozingatia mali, mitaji ya uendeshaji, huduma za kifedha kidijitali, bima, dhamana, mikopo ya vikundi ili kuongeza fursa za upatikanaji wa mitaji, hususan kwa wanawake na vijana.

Wataalamu hao walitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika warsha ya uenezaji wa maarifa na ushirikiano wa kifedha kwa ajili ya kusaidia mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi nchini.

Warsha hiyo iliandaliwa chini ya Mpango wa Kuwawezesha Kiuchumi Wanawake na Vijana katika Sekta ya Uvuvi kupitia Upatikanaji Shirikishi wa Masoko (WYEEFIMA), unaotekelezwa na Mastercard Foundation kwa kushirikiana na TradeMark Africa (TMA) na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Mkurugenzi wa TMA nchini, Elibariki Shammy, alisema sekta ya uvuvi inapaswa kuangaliwa kama mfumo mpana wa kiuchumi unahusisha wazalishaji wa pembejeo, wavuvi, wafugaji wa samaki, wakusanyaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na wachakataji.

Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha suluhisho za kifedha zinaendana na uhalisia wa biashara zinazofanyika katika mnyororo mzima wa thamani.

Shammy alisema biashara za uvuvi zinaweza kuwa za msimu na kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya wingi wa samaki na kuyumba kwa masoko, huku biashara nyingi ndogo zikikosa kumbukumbu sahihi za kifedha na dhamana.

“Sababu hizi ni miongoni mwa zinazoweza kuifanya sekta hii ionekane kuwa yenye vihatarishi kwa taasisi za fedha,” alisema, akitoa wito kwa taasisi hizo na wadau wa sekta ya uvuvi kufanya majadiliano ya wazi ili kupata suluhisho zinazotekelezeka.

Alisema sekta hiyo inahitaji mchanganyiko wa bidhaa za kifedha, ikiwemo mitaji ya uendeshaji, dhamana ya mali, huduma za kifedha kidijitali, bima, na ufadhili wa mnyororo wa thamani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi katika Wizara ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar, Musa Ramadhani Said, alisema kuna haja ya kuwaunganisha wadau wa sekta ya uvuvi na taasisi za fedha na kuanzisha mifumo ya mikopo inayozingatia mali walizonazo wavuvi pamoja na mazingira yao ya biashara.

Alisema kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee hakutoshi iwapo wadau hawatakuwa na fursa ya kupata huduma za uchakataji na masoko yenye tija ndani na nje ya nchi.

Said alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi ili kujenga mazingira wezeshi kwa biashara za uvuvi.

Naye, Dk Nazael Madala wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Tanzania Bara) alisema sekta ya uvuvi ina fursa kubwa kiuchumi, akibainisha kuwa kwa sasa inachangia asilimia 2.2 ya pato la taifa na inakua kwa wastani wa asilimia 6.2.

Alisema takribani watu milioni 6.5, sawa na karibu asilimia 10 ya Watanzania, wanahusika moja kwa moja au kwa njia nyingine katika shughuli zinazohusiana na uvuvi.

Dk Madala alisema upatikanaji mdogo wa fedha ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazozuia sekta hiyo kufikia uwezo wake kamili.

Alisema Serikali imeanza kushirikiana na taasisi za fedha kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu, akitolea mfano mpango uliozinduliwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza mwaka 2024 kwa ajili ya kusaidia ufugaji wa samaki kwa vizimba.

Chini ya mpango huo, alisema wakopaji waliweza kupata fedha bila kuhitajika kutoa dhamana ngumu ambazo kwa kawaida hutakiwa na benki.

Alisema mfumo huo umesaidia kuonyesha kuwa watu wasio na dhamana za kawaida wanaweza kufanya biashara za uvuvi kwa mafanikio wanapopatiwa msaada unaofaa wa kifedha.

Dk Madala alisema baadhi ya taasisi za fedha zimeanza kuanzisha huduma maalumu kwa ajili ya sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki, akizihimiza taasisi nyingine kuongeza bidhaa hizo.

Aidha, aliwataka watoa huduma za fedha kuangalia mnyororo mzima wa thamani, kuanzia uzalishaji, uhifadhi, usafirishaji, masoko hadi bima, badala ya kufadhili shughuli moja pekee.

Akifafanua kuhusu mpango wa WYEEFIMA, Meneja wa Upatikanaji wa Fedha wa mpango huo kutoka kampuni ya MicroSave Consulting, Elizabeth Gathu, alisema mpango huo pia utachunguza matumizi ya dhamana za vikundi kupitia vyama vya ushirika na jumuiya, kwa kuwa washiriki wengi hawana dhamana za kawaida zinazohitajika kupata huduma za kifedha.

Alisema mpango huo pia utahamasisha mikopo na bima ndogo ili kukabiliana na hatari zinazotokana na hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri biashara za uvuvi.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button