Serikali yasisitiza ushirikiano kukuza biashara Kigoma

KIGOMA: MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka wadau wa biashara na usafirishaji wanaotumia Bandari za Ziwa Tanganyika kuelekea nchi za Maziwa Makuu kushirikiana katika kuondoa changamoto zisizo za kikodi ili kuwezesha biashara kufanyika kwa tija kubwa.

Balozi Sirro aliyasema hayo mjini Kigoma katika kikao na wadau wa bandari kujadili changamoto zisizo za kikodi zinazojitokeza wakati wa usafirishaji wa shehena kwenda nchi za Maziwa Makuu kupitia Bandari ya Kigoma, akibainisha kuwa kila mdau akitimiza wajibu wake, utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) utakuwa na tija kubwa.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ,Dk.Baraka Mdima akizungumza katika kikao cha wadaau wa bandari kuzungumzia changamoto zisizo za kikodi

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua, alisema Serikali imejitahidi kutimiza wajibu wake kwa kuimarisha miundombinu ya bandari, usafirishaji majini na njia nyingine ili shehena zinazopitia Bandari za Ziwa Tanganyika ziweze kusafirishwa kwa tija.

Alisema changamoto zisizo za kikodi ni lazima zijadiliwe na kupatiwa ufumbuzi kwa pamoja, ili kila mdau aweze kushughulikia jambo linalomhusu.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma alisema Serikali imeuchagua Mkoa wa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati katika uchumi na biashara kuelekea soko la nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Dunia Shakuru, Mwenyekiti wa Mawakala wa Forodha Mkoa Kigoma

Alisema kila mdau, ikiwemo wasafirishaji wa shehena, mawakala wa forodha, wafanyabiashara na wasimamizi wa mamlaka za Serikali, ana wajibu wa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha azma ya Serikali ya kuufanya Kigoma kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi na biashara inatimia na kutoa tija katika shughuli za uchumi.

Awali, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dk. Baraka Mdima, alisema wadau wa bandari wana nafasi kubwa ya kuhakikisha TPA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ndiyo maana kikao hicho kimefanyika kujadili changamoto zisizo za kikodi na forodha na namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Dk. Mdima alisema kufanyika kwa kikao hicho si kwa bahati mbaya, bali kumelenga kuwakutanisha wadau wote wanaotumia bandari zinazosimamiwa na mamlaka hiyo kusafirisha shehena, ili kubaini changamoto zilizopo, kuzizungumzia na kupata ufumbuzi.

Wadau wa usafirishaji shehena kupiitia Bandari za Ziwa Tanganyika wakiwa kwenye kikao cha wadau wa bandari kujadili changamoto zisizo za kikodi zinazowakabili katika usafirishaji.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mawakala wa Forodha katika Bandari za Ziwa Tanganyika, Dunia Shakuru, alisema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari za Ziwa Tanganyika, bado zipo changamoto zisizo za kikodi ambazo zisipopatiwa ufumbuzi mapema zinaweza kuwa kikwazo kwa biashara.

Alisema changamoto hizo zinaweza kuchochea wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena kuhama na kutafuta njia nyingine za kusafirisha shehena zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button