Mnyeti ahoji zahanati ya kijiji kukosa dawa

GEITA: MKUU wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, ameeleza kushangazwa na taarifa ya Zahanati ya Kijiji cha Kihula, wilayani Chato, kukosa dawa muhimu aina ya paracetamol na amoxicillin.
Mnyeti ametoa kauli hiyo baada ya mzee mmoja, mkazi wa Kijiji cha Kihula, Kata ya Kasenga, kuwasilisha kero yake wakati wa mkutano wa hadhara, akidai kuwa zahanati hiyo haina dawa.
Akiwasilisha kero yake katika mkutano huo, mzee huyo alimkabidhi Mkuu wa Mkoa daftari la matibabu kama ushahidi, likionyesha maelekezo ya daktari yaliyomtaka kwenda kununua dawa hizo kutokana na kukosekana katika zahanati hiyo.
Mnyeti amesema inashangaza kuona zahanati ya kijiji inakosa dawa muhimu kama hizo ingali taarifa zinaonyesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya afya vya serikali umeimarika.
“Amoxicillin ni kitu cha kukosa kweli, panadol haipo kweli, mtu anaambiwa akanunue kwenye duka la dawa, huo uhuni sitaki kwenye mkoa huu, DMO tutagombana sana.
“Mimi sitaki wananchi hawa wakae kulalamika, serikali hii inaleta zaidi ya asilimia 90 ya dawa kwenye vituo vyake, zinapotelea wapi”, amehoji Mnyeti.
Mnyeti ameagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chato (DMO) kuhakikisha kamati za zahanati na vituo vya afya zinashirikishwa katika mapokezi, ukaguzi na usimamizi wa dawa na vifaa tiba.
“Kamati iwepo na ikague hizo dawa zinapoingia, kamati ya kituo cha afya ijue dawa zimekuja ngapi na ni aina gani”, amesema Mnyeti.
DMO wa Chato, Dk Daniel Mzee amekiri kuwa kila kituo cha afya kina kamati mbili ambazo ni kamati ya kituo cha afya pamoja na kamati ya mapokezi ya dawa na zinaendelea kushirikishwa.
Amesema changamoto ya upungufu wa dawa hizo huenda ilitokana na mahitaji makubwa ya wananchi lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinatumika kwa usahihi.



