Brela yawafikia wafanyabiashara kupitia kliniki

ARUSHA: Wakala Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umesogeza huduma zake karibu na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Arusha kupitia Kliniki ya Viwanda na Biashara, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uelewa kuhusu urasimishaji wa biashara.
Akizungumzia umuhimu wa kliniki hiyo inayofanyika kwa siku tatu katika Viwanja vya Ngarenaro, Jijini Arusha, Ofisa Leseni wa BRELA, Rajab Chambega, amesema imekuwa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi, kuwapatia huduma na kutoa elimu kuhusu taratibu za usajili na uendeshaji rasmi wa biashara.

Amesema kliniki hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi wa Arusha na maeneo jirani, ili waweze kupata huduma na ufafanuzi wa masuala mbalimbali moja kwa moja kutoka kwa maafisa wa taasisi husika.
Chambega amesema BRELA inatoa huduma mbalimbali kupitia kliniki hiyo, zikiwamo leseni za biashara za kundi A, leseni za viwanda, usajili wa alama za biashara na huduma, majina ya biashara pamoja na kampuni.

Amesema ushiriki wa BRELA katika kliniki hiyo umekuwa na manufaa kwa taasisi hiyo na wananchi kutokana na fursa ya kuwahudumia wateja, kutoa elimu na kujibu maswali yanayohusu taratibu za usajili na upatikanaji wa leseni za biashara.
“Lengo kuu hasa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma zetu. Tumepata fursa ya kutoa elimu kwa wananchi na wakazi wa Arusha, hususan katika masuala ya leseni, biashara na makampuni,” alisema.
Ameeleza kuwa pamoja na huduma zinazotolewa katika kliniki hiyo, BRELA imeboresha mifumo yake ya kidijitali ili kuwawezesha wateja kupata huduma kwa urahisi bila kulazimika kufika katika ofisi za wakala huo.

Chambega amesema mifumo hiyo imeboreshwa ili kuwa rafiki zaidi kwa watumiaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma za BRELA kupitia simu za kiganjani.
Amesema utoaji wa elimu kwa wananchi pia unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kufahamu mahitaji na nyaraka zinazohitajika kabla ya kuomba huduma, hatua inayoweza kurahisisha taratibu za usajili na utoaji wa leseni.



