Umasikini, elimu, imani potofu vinavyochochea udumavu Katavi

KATAVI; Udumavu kwa watoto mkoani Katavi hauchangiwi na sababu moja pekee. Ushahidi kutoka kwa wazazi, wataalamu wa afya na viongozi unaonesha mchanganyiko wa hali ya kiuchumi ya kaya, uelewa wa lishe, namna chakula kinachozalishwa kinavyotumika, pamoja na imani na mitazamo kuhusu chakula na malezi ya watoto.

Kwa mujibu wa Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey (TDHS-MIS) 2022, asilimia 32.2 ya watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Katavi wana udumavu, kiwango kilicho juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 30.0. Hata hivyo, kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 38.8 mwaka 2015/16.

Umasikini unapunguza uwezo wa familia kulisha mtoto

Kwa baadhi ya familia, tatizo huanza kwenye kipato. Elizabeth Shija Kamsanga, mkazi wa Halmashauri ya Tanganyika, ambaye mtoto wake alikuwa akipatiwa matibabu ya udumavu katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, anaeleza kuwa alipata elimu kuhusu vyakula anavyopaswa kumpa mtoto, lakini uwezo wa kifedha ulimzuia kutekeleza ushauri huo wakati wote.

“Walituambia tule mboga, samaki na vyakula vingine, lakini sikuweza kuvipata,” anasema.

Hali hiyo inaonesha kwamba uelewa wa lishe pekee hauondoi tatizo ikiwa familia haina uwezo wa kiuchumi wa kufikia baadhi ya vyakula.

Tatizo la lishe katika familia hiyo halikuonekana kwa mtoto pekee. Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Dk. Paul Swakala, Elizabeth mwenyewe alikuwa na hali ya utapiamlo kwa mtu mzima (Adult Malnutrition).

Ushahidi mwingine unatoka kwa Evalina John, mzazi wa Paskali Salumu, ambaye alieleza changamoto za mtoto wake pamoja na hali ya kipato ya familia yake licha ya kujishughulisha na kilimo cha mahindi na karanga. Familia hiyo ililima takribani ekari tatu za mahindi na ekari moja ya karanga, lakini sehemu kubwa ya mazao iliyopatikana ilitumika katika mahitaji ya familia na hali ya kifedha ikaendelea kuwa ngumu.

Hali hizi zinaonesha kuwa tatizo la lishe haliishii kwenye uwepo au ukosefu wa chakula nyumbani. Pia linahusu uwezo wa kaya kupata mlo wenye mchanganyiko wa vyakula unaohitajika kwa ukuaji wa mtoto.

Nuru Magembe na Mama Mehmet, miongoni mwa wazazi waliohojiwa, pia walieleza changamoto zinazohusiana na uwezo wa familia kumudu mahitaji muhimu ya lishe.

Takwimu za Household Budget Survey 2017/18 zinaonyesha Katavi ilikuwa na kiwango cha umasikini wa mahitaji ya msingi cha asilimia 30.7, ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 26.4.

Hivyo, familia na mazingira yake ya kiuchumi ni miongoni mwa wahusika wakuu katika mnyororo wa sababu unaoweza kumweka mtoto katika hatari ya udumavu.

Chakula kinazalishwa, lakini mtoto anapata nini?

Katavi ni mkoa unaotegemea kwa kiasi kikubwa kilimo. Uzalishaji wa mazao ya chakula uliongezeka kutoka tani 990,629 mwaka 2021 hadi tani 1,286,905 mwaka 2025, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Mkoa wa Katavi.

Lakini uwepo wa chakula kwa wingi mkoani haujibu moja kwa moja swali la kama mtoto anapata mlo wenye virutubisho anavyohitaji.

Kwa mkulima, mazao yanaweza kuwa chakula na wakati huo huo kuwa chanzo cha kipato. Sehemu ya mavuno inaweza kuuzwa ili kugharamia mahitaji mengine ya familia, na kiasi kinachobaki ndicho hutumika nyumbani.

Ofisa Lishe wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Neema Kambi, anasema, baadhi ya watoto hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa, wakati hali zao tayari imekuwa mbaya. Baadhi yao huanza kutibiwa kwa njia za jadi kabla ya kufikishwa hospitalini, huku wengine wakichelewa kutokana na hali ya kipato ya familia.

Anaongeza kuwa baadhi ya familia huamini mtoto akipewa chakula kingi ameshiba bila kuzingatia kama chakula hicho kina virutubisho vinavyohitajika kulingana na umri wake. Hivyo, kwa Neema, changamoto haipo tu kwenye kiasi cha chakula kinachopatikana, bali pia aina ya chakula anachopewa mtoto na namna kinavyotayarishwa na kutumiwa katika familia.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, anaeleza kuwa changamoto ipo pia katika namna jamii inavyotumia chakula kilichopo.

“Changamoto tuliyonayo ni namna ya ulaji na jamii kubadilika. Watu kuelewa kwamba kula si kujaza tumbo au kushiba, unatakiwa ule lakini uchanganye.”

Hapa sekta ya kilimo na mifugo, familia na Serikali zinakutana katika mnyororo mmoja: chakula kuzalishwa, kufikishwa kwenye kaya na hatimaye kutumiwa kwa namna inayokidhi mahitaji ya mtoto.

Mifugo ipo, lakini virutubisho havifiki kwa mtoto

Tatizo hilo linaonekana pia katika mifugo.

Mbali na kilimo, Katavi ina sekta kubwa ya mifugo. Kwa mujibu wa Tovuti rasmi ya Mkoa wa Katavi, uzalishaji wa maziwa mkoani humo umeongezeka kutoka lita milioni 19.2 mwaka 2021 hadi lita milioni 23 mwaka 2025, wakati uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 450,005 hadi tani 983,360 katika kipindi hicho.

Taarifa hiyo, iliyochapishwa Machi 4, 2026, inaeleza pia kuwa sekta ya mifugo imepata zaidi ya Sh bilioni 1.5 hadi Juni 2025 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma za mifugo.

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha kiwango cha uzalishaji, si kiasi cha nyama au maziwa kinachotumiwa na kaya. Hivyo, bado kuna pengo la taarifa kuhusu kiwango ambacho bidhaa hizo zinafika kwenye meza za familia, hasa kwa watoto.

Imani potofu huathiri uchaguzi wa chakula

Mbali na uchumi, imani na mitazamo ya jamii ni sababu nyingine inayoweza kuathiri lishe ya mtoto.

Jamila anaeleza kuwa baadhi ya wanawake wajawazito hukutana na imani zinazowafanya waepuke aina fulani za vyakula kwa hofu kwamba vinaweza kumdhuru mtoto. Pia, baadhi ya wazazi hawafuati kikamilifu ushauri kuhusu unyonyeshaji na malezi ya watoto.

Ofisa Lishe wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Neema Kambi, anatoa mifano ya familia zinazofuga kuku lakini haziwapi watoto mayai, zinazofuga ng’ombe lakini huuza maziwa badala ya kuwapa watoto, pamoja na wazazi wanaowanyima watoto baadhi ya vyakula kama kumbikumbi na matunda kutokana na imani mbalimbali.

Hivyo, wazazi na jamii kwa ujumla wana nafasi kubwa katika namna mtoto anavyopata chakula, lakini pia viongozi wa dini, wataalamu wa afya na lishe wana nafasi katika kujenga uelewa unaoweza kubadili mitazamo hiyo.

Elimu ya lishe: nani anapaswa kuhakikisha inamfikia mzazi?

Katika kukabiliana na hali hiyo, elimu ya lishe hutolewa kupitia vituo vya afya na mikutano ya vijiji na mitaa.

Kwa mujibu wa Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo,Jackline Kitomari vikao vya SALIKI (Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji) vinalenga kuwafundisha wananchi kuhusu afya na lishe kwa kutumia mifano ya vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao.

Anasema vikao hivyo vilipoanza mwaka 2023, baadhi ya mikutano ilikuwa ikihudhuriwa na watu watano hadi saba, wengi wao wakiwa wanawake. Kwa sasa, baadhi ya mikutano hufikisha washiriki kati ya 50 na 70.

Katika vikao hivyo wananchi huonyeshwa kwa vitendo namna ya kuandaa mlo na wakati mwingine hushiriki kula chakula kilichoandaliwa. Njia hiyo imekuwa muhimu kwa sababu wananchi hawaishii kusikiliza elimu, bali huona kwa vitendo namna vyakula mbalimbali vinavyoweza kuchanganywa.

Hata hivyo, changamoto ya msingi inabaki kwa kaya yenye uwezo mdogo wa kiuchumi, kwa sababu elimu pekee haiwezi kumwezesha mzazi kununua chakula ambacho hana uwezo nacho.

Waganga wa tiba asilia nao ni sehemu ya mnyororo

Sababu nyingine inayotajwa na wataalamu ni kuchelewa kwa baadhi ya watoto kupata huduma sahihi. Seleman Hamisi, Afisa Lishe Mkoa wa Katavi, anasema baadhi ya familia huanza kuwapeleka watoto kwa waganga wa jadi kabla ya kufika katika vituo vya afya, na wakati mwingine watoto hufikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya zaidi.

Hii inaweka familia na watoa huduma za tiba katika nafasi muhimu ya kuhakikisha mtoto mwenye dalili anapata huduma sahihi kwa wakati. Pia inaonyesha kwa nini mapambano dhidi ya udumavu hayawezi kuachwa kwa sekta ya afya pekee.

Utafiti zaidi unahitajika

Ofisa Lishe Mkoa wa Katavi, Seleman Hamisi, anasema baadhi ya sababu za tatizo hilo tayari zinajulikana, ikiwemo ulaji usio na mchanganyiko na kutokidhi idadi inayofaa ya milo. Hata hivyo, anasema bado kuna haja ya kufanya tafiti za kina ili kubaini sababu nyingine zilizo nyuma ya tatizo hilo.

Kwa sababu hiyo, halmashauri zimeanza kuelekezwa kutenga fedha kwa ajili ya tafiti zitakazosaidia kubaini visababishi mahsusi vya changamoto za lishe katika maeneo yao.

Seleman pia anataja kuchelewa kwa watoto kupata huduma sahihi kutokana na baadhi ya familia kukimbilia kwa waganga wa jadi kabla ya kufika katika vituo vya afya. Kwa mujibu wake, baadhi ya watoto hufikishwa hospitalini wakiwa katika hatua mbaya zaidi baada ya kuanza kutibiwa nje ya mfumo rasmi wa afya.

Anaona ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, jamii na viongozi wa dini kuwa muhimu katika kuongeza uelewa kuhusu lishe na kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto kwenye huduma za afya mapema wanapoona dalili za tatizo.

DC aeleza hatua za uwajibikaji

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, anasema Serikali haishii kutoa elimu, bali inafuatilia pia utekelezaji wa mikakati ya lishe kupitia vikao vya Kamati ya Lishe.

Anasema pale halmashauri inapopata alama nyekundu au njano katika vigezo vinavyotumika kupima utekelezaji, suala hilo hujadiliwa na maafisa lishe, Mkurugenzi wa Halmashauri na watendaji husika. Kwa mujibu wake, maonyo hutolewa kwa watendaji na wasimamizi pale inapobainika kuwa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Jamila anasema ofisi yake imekuwa ikiwakumbusha watendaji kutekeleza wajibu wao, huku hatua za kiutawala zikibaki chini ya mamlaka husika za halmashauri. Anaeleza pia kuwa Kamati ya Lishe ya Wilaya hufuatilia changamoto zinazojitokeza katika vikao vya kila robo mwaka.

Kwa mujibu wa Jamila, mfumo huo wa kufuatilia utekelezaji kwa kutumia vigezo na alama umechangia mabadiliko katika utekelezaji wa afua za lishe. Ingawa hakutoa takwimu za kulinganisha kipindi cha miaka mitatu iliyopita, anasema anaona mabadiliko katika mwaka jana na mwaka huu.

Udumavu ni jukumu la nani?

Ushahidi huu unaonesha kuwa udumavu hauwezi kueleweka kwa kumtazama mzazi pekee. Familia ina wajibu wa namna mtoto anavyolishwa. Sekta ya kilimo na mifugo ina nafasi katika uzalishaji wa chakula na bidhaa za mifugo. Wataalamu wa afya na lishe wana jukumu la elimu, uchunguzi na huduma. Viongozi wa dini na jamii wanaweza kuathiri mitazamo kuhusu chakula. Waganga wa tiba asilia wanaweza kuathiri muda ambao mtoto anafikishwa kwenye huduma rasmi. Na Serikali na halmashauri zina wajibu wa kupanga, kugharamia, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa afua za lishe.

Kwa Katavi, changamoto kubwa si uzalishaji wa chakula pekee. Ni mnyororo mzima unaoanzia kwenye kipato cha kaya, uzalishaji wa chakula, matumizi yake, imani na uelewa wa lishe, hadi upatikanaji wa huduma kwa wakati.

Kwa kiwango cha udumavu cha asilimia 32.2, kila kiungo katika mnyororo huo kina nafasi katika kueleza kwa nini mtoto anadumaa, na kwa hiyo kila mmoja ana sehemu ya kuwajibika.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button