Namtumbo mambo safi matumizi nishati safi

RUVUMA; Kampuni ya Oryx Gas imekabidhi mitungi ya gesi 600 na vifaa vyake kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.
Oryx Gas imetoa mitungi hiyo ya gesi kwa wananchi hao kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera kwa lengo la kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini, ili kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Iman Mtafya, Meneja Fedha wa kampuni hiyo Ashery Mbasha, amesema kupitia uwezeshaji huo Oryx Gas inaendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
“Wilaya ya Namtumbo, kama ilivyo kwa maeneo mengi nchini Tanzania, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya matumizi makubwa ya kuni na mkaa. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.

“Hivyo kama hatua madhubuti hazitachukuliwa, vizazi vijavyo vinaweza kukumbana na uhaba mkubwa wa rasilimali za misitu na athari za mabadiliko ya tabianchi,”amesema na kuongeza kwa kutambua changamoto hiyo, Oryx Gas imeamua kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuhamasisha matumizi ya gesi ya LPG kama mbadala wa kuni na mkaa.
Amesisitiza matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza moshi majumbani, kuokoa muda wa kupika na kuongeza ubora wa maisha kwa ujumla.
Mbasha amesema dhamira ya Oryx Gas ni kuhakikisha Tanzania inafikia mabadiliko kamili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Wilaya ya Namtumbo ni moja ya maeneo ambayo tumeyawekea kipaumbele katika safari hii muhimu.

“Oryx Gas pia imekuwa mshirika wa maendeleo katika wilaya hii ya Namtumbo kupitia miradi mbalimbali ya nishati safi.
“Miongoni mwa mafanikio hayo ni ufungaji wa mfumo wa hifadhi na usambazaji wa gesi ya LPG katika Shule ya Wasichana ya Samia Suluhu, hatua iliyowezesha taasisi hiyo kutumia nishati safi kwa manufaa ya wanafunzi na watumishi wake.”
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi wa Namtumbo hasa waliopata mitungi ya gesi ya Oryx kutumia majiko hayo kwa usalama na kuendelea kueneza elimu ya matumizi ya gesi ya LPG katika jamii zenu. Kwa pamoja tunaweza kujenga Namtumbo yenye mazingira bora, afya bora na maendeleo endelevu.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ,ambaye pia ni waziri wa Katiba na sheria Dk.Juma Homera ameishukuru kampuni ya Oryx kwa kuwapatia majiko 600 na kati hayo majiko 215 yamekabidhiwa kwa wananchi wa Namtumbo na mengine yatapelekwa na kugawanywa kila kata kwa wananchi wa wilaya hiyo.



