Wasafiri SGR kupata huduma uchunguzi magonjwa ya moyo

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeandaa mpango wa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na yasiyoambukiza ndani ya treni ya SGR, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani Septemba 29.
Huduma hiyo inatarajiwa kufanyika Septemba 21 hadi 27 mwaka huu, ambapo wananchi watakaotumia usafiri wa SGR watapata fursa ya kupimwa afya ya moyo bila malipo wakati wa safari.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema hatua hiyo inalenga kufikia wananchi kwa urahisi zaidi na kuhakikisha wanapata huduma za afya, upendo na matumaini ya kuishi.
Amesema vipimo hivyo ambavyo kwa kawaida vinaweza kugharimu hadi Sh 500,000 katika hospitali, vitatolewa bure ndani ya treni kwa wananchi watakaoshiriki mpango huo.
“Tunataka kuhakikisha wananchi wanapata upendo na matumaini ya kuishi. Tutakuwa na huduma za upimaji wa moyo na magonjwa yasiyoambukiza ndani ya SGR, na mtu atakayebainika kuwa na tatizo atachukuliwa hatua za matibabu,” amesema.
Aidha, amesema mpango wa kuwa na huduma za hospitali ndani ya treni hauishii katika maadhimisho hayo, bali unalenga kuwa huduma endelevu kwa wananchi wanaosafiri kwa SGR.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema wanaendelea kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya ndani ya treni, ikiwemo kufanya marekebisho maalumu katika baadhi ya mabehewa.
Amesema mpango huo unaweza kusaidia wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine, kwa kuwa mabehewa hayo yatakuwa na vitanda na mazingira ya kuwezesha wagonjwa kuendelea kupata huduma wakati wa safari.
“Tunajaribu kuangalia mazingira ya hospitali zetu na namna mabehewa yanavyoweza kufanyiwa marekebisho ili kusaidia wagonjwa wanaosafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Mabehewa yanaweza kuwa na vitanda na wagonjwa wakaendelea kupata matibabu tofauti na kusafirishwa kwa magari ya wagonjwa,” amesema.
Ameongeza kuwa kutakuwa na behewa maalumu kwa ajili ya watu wanaohitaji huduma za matibabu, ambapo wataweza kufanyiwa vipimo na kuendelea kupata huduma wakiwa ndani ya SGR.
“Mpango huo unalenga pia kuunganisha usafiri wa reli na huduma za afya, huku wananchi wakipewa fursa ya kupata uchunguzi wa afya bila kulazimika kusubiri hadi wafike hospitalini.



