Dk Norga Komba: Utekelezaji Ilani CCM unagusa wananchi

CHINA: Dk Norga Komba, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini China, anasema kwa mtazamo wake, utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika kipindi hiki unaonekana katika maeneo mbalimbali yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan nishati, miundombinu, uwekezaji, elimu, afya na huduma za kijamii.
Katika sekta ya nishati, Dk Komba anaeleza kuwa kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere ni hatua muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania.
“Mradi huo una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na una nafasi kubwa katika kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme, sambamba na kuwezesha shughuli za uzalishaji na uwekezaji,” anasema.
Kwa upande wa uwekezaji, anaona Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayochochea uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Ukuaji wa uwekezaji, kwa mtazamo wake, una maana pana kwa wananchi kwa sababu unasaidia kupanua shughuli za uzalishaji, kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na za kati, na kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa.
“Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa mwaka 2025 pekee zilisajiliwa zaidi ya miradi 900 ya uwekezaji, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika uchumi wa Tanzania,” anasema.
ANASEMAJE KWENYE SEKTA YA AFYA
Akizungumzia mafanikio makubwa ambayo anaona Serikali imeyapata katika kuboresha maisha ya wananchi, Komba ametaja sekta ya elimu kuwa miongoni mwa maeneo muhimu.
Anasema Serikali imeendelea kuwekeza katika upanuzi wa upatikanaji wa elimu, miundombinu ya shule na vyuo, pamoja na mikopo ya elimu ya juu.
“Hatua hizi zimewezesha Watanzania wengi zaidi kupata nafasi ya kusoma na kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye,” anasema Dk Komba.
Kwa mujibu wake, Serikali pia imeendelea kutoa elimu ya msingi bila malipo na kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu.
Katika sekta ya afya, amesema uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali, dawa, vifaa tiba na huduma za afya umeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi.
“Hili ni eneo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa sababu afya bora ndiyo msingi wa uzalishaji na ustawi wa familia,” anasema.
VIPI KUHUSU MIUNDOMBINU NA NISHATI
Dk Komba pia anataja miundombinu ya usafirishaji kuwa eneo jingine ambalo ameona mafanikio.
Anasema ujenzi na upanuzi wa barabara, madaraja, reli ya SGR na miundombinu ya usafiri wa anga umeongeza muunganiko wa maeneo mbalimbali nchini na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
“Miradi kama SGR na miundombinu ya kisasa ya usafiri pia ina umuhimu mkubwa katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema.

Katika eneo la nishati, Komba anaeleza kuimarika kwa miundombinu ya umeme na utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme, hususan Bwawa la Julius Nyerere, kunaweka msingi wa uchumi unaotegemea uzalishaji na viwanda.
CHANGAMOTO YA MAWASILIANO
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo, Komba anaeleza kuna changamoto ambazo bado zinahitaji Serikali kuongeza nguvu katika kuzitatua.
Anafafanua suala la mawasiliano ya taarifa za utekelezaji wa miradi na fursa zinazotolewa na Serikali kuwafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.
“Serikali inaweza kuwa inatekeleza miradi na programu nyingi nzuri, lakini kama taarifa zake hazimfikii mwananchi kwa wakati, kuna hatari ya wananchi kutonufaika kikamilifu na fursa hizo au kutokuwa na uelewa wa hatua zinazochukuliwa,” anasema.
Kwa hiyo, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha zaidi mifumo ya mawasiliano ya Serikali kwenda kwa wananchi, hususan katika ngazi za vijiji, mitaa, kata na halmashauri.
Anasema matumizi ya teknolojia, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na viongozi wa jamii yanaweza kusaidia kufikisha taarifa kwa haraka zaidi.
“Nadhani tunahitaji kwenda hatua moja zaidi: siyo tu Serikali kutoa taarifa kwamba mradi umejengwa, bali kueleza wazi mradi huo umeleta faida gani, nani amenufaika, changamoto zilizopo na nini kinachofuata,” Anaeleza.
Kwa mtazamo wake, hatua hiyo itaongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi.
“Serikali yenyewe imetambua umuhimu wa taarifa za maendeleo kuwafikia wananchi kwa wakati katika mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” anahitimisha.
ANAZUNGUMZIAJE SEKTA YA KILIMO
Norga Komba anasema Serikali imeendelea kuwekeza katika umwagiliaji, upatikanaji wa mbegu bora, mbolea, huduma za ugani, mechanisation na matumizi ya teknolojia za kisasa. Pia kuna jitihada za kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mnyororo wa thamani.
Kwa mfano, katika mwaka 2024/2025, uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia takribani tani milioni 23.78, kutoka tani milioni 22.8 mwaka uliotangulia. Wizara pia imeweka mkazo katika kuimarisha huduma za ugani na kuhamisha teknolojia kutoka kwa watafiti kwenda kwa maafisa ugani na wakulima.
“Lakini hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba mkulima anapata faida zaidi kutoka kwenye kilimo. Hii inahitaji kupunguza gharama za uzalishaji, kuimarisha uhifadhi baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao, upatikanaji wa masoko na kuhakikisha mkulima anaingia kikamilifu katika kilimo biashara,” anasema Norga Komba.
MTAZAMO WAKE FURSA KWA WATANZANIA
Katika eneo hili, Norga Komba anasema Serikali imechukua hatua kadhaa muhimu, hasa kupitia uwezeshaji wa vijana, wanawake na wajasiriamali.
Anasema mikopo na programu mbalimbali za uwezeshaji zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kuanzisha au kupanua biashara zao na hivyo kujenga uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine.
Ametaja vijana na wanawake kuwa wamefikiwa kwa kiwango kikubwa kupitia mikopo na programu mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi.

“Hata hivyo, suala la ajira linahitaji kuangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi kuliko ajira za Serikali pekee. Tunahitaji uchumi unaozalisha ajira kupitia uwekezaji, viwanda, kilimo cha kisasa, teknolojia, biashara, nishati, utalii na huduma mbalimbali,” anafafanua.
Anazungumzia pia upande mwingine, diplomasia ya Tanzania kuwa imeendelea kufungua milango ya fursa kwa Watanzania. Anasema Mahusiano mazuri na nchi mbalimbali yamekuwa yakitoa nafasi katika biashara, uwekezaji, elimu, mafunzo, teknolojia na ushirikiano wa kitaalamu.
Hivyo, diplomasia ya kiuchumi inaweza kuwa chombo muhimu zaidi cha kuwaunganisha vijana na wanawake wa Tanzania na masoko, mitaji, teknolojia na maarifa kutoka nje.


