NGO’s zatakiwa kuacha kutegemea wafadhili

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’s) yametakiwa kubuni miradi ya kujiongezea kipato ili kuachana na utegemezi wa wafadhili ambao wakati mwingine misaada hiyo ina ajenda hasi na mipango ya serikali.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani hapa.

Alisema utegemezi huo huyafanya mashirika hayo kutekeleza

miradi kwa kufuata matakwa ya wafadhili, badala ya malengo na vipaumbele vya nchi hali ambayo wakati mwingine kuwa na miradi ambayo sio endelevu.

Aidha, alisema ukosefu wa misingi ya uwazi na uwajibikaji wa baadhi ya mashirika hayo katika utendaji kazi kwa kutotoa taarifa zao kwa serikali hali ambayo imekuwa ikileta taswira mbaya kwa sekta hiyo kwa kuonekana yanajinufaisha yenyewe.

“Ukosefu wa uwazi umesababisha baadhi ya mashirika kutakatisha fedha haramu, kutumia jina la nchi vibaya na kutoa taarifa zinazopotosha jamii,” alibainisha.

Mkuu wa mkoa aliyataka mashirika hayo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata mwongozo wa uratibu wa mashirika hayo ya mwaka 2020 ambao unaelekeza kufanya kazi kwa ukaribu na serikali.

Vilevile aliwaagiza watendaji wa serikali kuendelea kufanya tathmini kwa mashirika hayo ili kubaini vihatarishi kwa sekta hiyo ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza ikiwamo matumizi mabaya ya vyanzo vya fedha.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mashirika hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tanga, Glory Maleo alisema mashirika hayo yanakabiliwa na ukosefu wa wataalamu wa uandishi wa miradi, hali ambayo husababisha kukosa fursa za kupata fedha kwa ajili ya maendeleo yao.

“Kuna tatizo la wataalamu kukosa elimu ya uandishi mzuri wa michanganuo ya miradi ambayo inawapatia fedha za utekelezaji pamoja na mwongozo wa uratibu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali uliotolewa mwaka 2020, haufahamiki vizuri kwa wadau ambao ni wamiliki wa mashirika hayo,” alisema.

Maleo alisema pamoja na matatizo ya kifedha mashirika yamefanikisha utoaji wa elimu mbalimbali kwa jamii na kufanya kampeni za kuzuia mila na desturi zinazofifisha maendeleo, kama vile kuzuia matumizi ya dawa za kulevya.

Alibainisha kwamba katika Mkoa wa Tanga kuna jumla ya mashirika 271 yanayofanya kazi, lakini 152 ndiyo yanatoa taarifa za utekelezaji wa shughuli zake kwa kipindi cha robo mwaka.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button